Katibu Mkuu Maganga awataka watafiti, kuweka mipango ya matumizi ya rasilimali za bahari

Mar, 27 2023

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga ametoa wito kwa watafiti, wataalamu na wanasayansi ya bahari kujadili kwa pamoja namna bora ya kutunza, kusimamia na kuwekeza katika rasilimali za bahari zilizopo nchini ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ametoa wito huo leo Machi 27, 2023) jijini Dar es Salaam wakati akifungua Warsha ya Uhakiki wa Taarifa ya Upembuzi yakinifu wa awali kuhusu Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Bahari (MSP) kwa Nchi za Magharibi mwa Bahari ya Hindi iliyoandaliwa na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Bi. Maganga amesema kuwepo kwa mpango shirikishi wa matumizi ya maeneo ya bahari ni sehemu ya suluhisho la kuleta matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa kuzingatia utunzaji sahihi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“kuna fursa nyingi katika matumizi ya Bahari ambazo zikifanyika kwa namna endelevu zitachangia katika ukuaji wa Uchumi. Shughuli kama vile uvuvi mdogo, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji samaki na mazao ya baharini zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Buluu na hatimaye kukuza uchumi wa nchi” amesema Bi. Maganga.

Aidha ameeleza kuwa Malengo ya Umoja wa Mataifa hasa lengo Namba 14 la Maendeleo Endelevu linasisitiza matumizi endelevu ya bahari, ambapo lengo hilo linakwenda sambamba na malengo ya warsha hiyo inayohimiza kupitia na kuhakiki taarifa ya upembuzi yakinifu wa awali wa Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Bahari.

Akifafanua zaidi Maganga amesema kuwa Mpango huo umekuja katika wakati mwafaka ambapo Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar zikiwa zimejipanga katika kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili ujenga uchumi imara.

Ameongeza kuwa mafanikio ya Uchumi wa Buluu yanategemea uwepo kwa Mpango Mahsusi wa Matumizi ya Maeneo ya Bahari, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar zitaendelea kushirikiana na wadau katika kuratibu na kushiriki katika utekelezaji wa Mpango huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la The Nature Conservancy kutoka Ujeruamani Bi. Lucy Maghembe amesema washa hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya sayansi ya bahari waliokutana kwa ajili ya kujadili sera na mipango endelevu ya usimamizi wa rasilimali za bahari na namna bora ya kushughulikia migongano ya matumizi ya rasilimali za bahari.

“Katika Afrika Tanzania tunakuwa taifa la nne kuwa na Mpango wa aina hii. Mataifa mengine ya Kenya, Shelisheli na Mauritius zimeanza utekezaji wa Mpango huu. Tumejipanga kuja na sera na mipango imara itakayosaidia usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari katika ukanda wa bahari ya Hindi.

Naye Mtaalamu wa Sayansi ya Bahari, Profesa Yunus Mgaya amesema wa wanasayansi umebaini kuongezeka kasi ya matumizi ya rasilimali za bahari katika Ukanda wa Bahari ya Hindi hatua inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwemo nishati, gesi, utalii n.k

“Utafiti uliofanyika umetoa mapendekezo ya kuwa na mifumo ya kitaasisi inayosaidia usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za bahari ili kuweza kuzuia migogoro na migongano baina ya watumiaji wa rasilimali zilizopo baharini” amesema Prof. Mgaya.

Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Uchumi wa Buluu, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Zahor Alharousy amesema kupitia Mpango huo uliobuniwa na wataalamu utaiwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupanua wigo na fursa za ukuaji wa uchumi kwa wananchi hususani wavuvi na wakulima wa zao la mwani.

Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha Mpango unaondaliwa unakuja na mipango endelevu ya matumizi ya rasilimali za bahari na kuibua fursa kwa wakulima na wavuvi"

Warsha hiy imeandaliwa na Shirika la The Nature Conservancy (TNC) kutoka Nchini Ujeremani inashirikisha wadau, wafadhili na mashirika ya kimataifa yanaohusika katika usimamizi, matumizi na uwekezaji katika fukwe za bahari, maziwa na mito.

Settings