Katibu Mkuu Maganga ahimiza utunzaji uoto wa asili kuhifadhi mazingira

Feb, 29 2024

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga amewataka wananchi wa Vijiji vya Magubike na Ilalasimba vilivyopo Kata ya Nzihi Halmashauri ya Iringa Vijijini, Mkoani kufanya shughuli zisizoharibu mazingira ili kutunza uoto wa asili wa maeneo hayo.

Ameyasema hayo Februari 28, 2024 wakati alipoongoza Ujumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) kukagua shughuli za utekelezaji wa Mradi katika Kata ya Nzihi, Halmashauri ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa.

Katibu Mkuu Bi. Maganga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mradi wa SLR, alikagua shughuli za hifadhi wa mazingira katika Kata hiyo ikiwemo hifadhi ya msitu wa Kijiji cha Ilalasimba, Shamba darasa la kilimo hifadhi, shamba darasa la malisho Kijiji cha Ilalasimba, shughuli za ufugaji ng’ombe wa maziwa na hifadhi ya Kijiji cha Magubike.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa uoto wa asili katika maeneo yote ya Mradi, Serikali kupitia Mradi wa SLR imeunda timu ya Wataalamu kutoka Wizara za Kisekta zikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maji ikiwa ni mkakati mahsusi wa kurudisha uoto wa asili uliopotea katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kwa sisi wa zamani sote ni mashahidi tunakumbuka hali ya maeneo haya ilivyokuwa na uoto wake wa asili tofauti na hali ilivyo sasa…..Ili kurejesha uoto wa asili wa eneo hili tumeleta Mradi huu wa SLR na matunda yameanza kuonekana sasa, tunataka mradi huu uwe wa mfanotusimulie hadithi nzuri kwa vizazi vyetu” Amesema Katibu Mkuu Maganga.

Aidha ameipongeza Timu ya Watalaamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi ikiwemo upandaji wa miti kwa mujibu wa maelekezo ya Serikal ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu Bi. Maganga amesema kuwa ni muhimu shughuli za kilimo, mifugo na misitu ziende sambamba na juhudi za hifadhi ya mazingira ili kuhakikisha mradi huounakuwa endelevu na hivyo kuendelea kutunza uoto wa asili wa maeneo hayo.

Aidha ameridhishwa na mwamko wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya mazingira, hatua iliyotokana na jamii hizo kuwa mstari wa mbele kusimamia miradi katika kujikwamua kiuchumi na hivyo kuongeza pato la familia.

Amefafanua kuwa uoto wa asili sambamba na upandaji wa miti pia unahusisha utumiaji wa rasilimali zilizopo kwa njia endelevu ikiwa ni pamoja na kuacha maeneo yaliyoharibika kurejesha yenyewe uoto wake wa asili na kuachana na shughuli zinazopelekea uharibifu ikiwemo ukataji miti.

Settings