Kamishna TFS: Ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuifanya Tanzania ya Kijani

Apr, 09 2024
Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini, SACC James Nshare amesema ushirikiano mkubwa kati ya TFS na Ofisi ya Makamu wa Rais unasaidia kutimiza lengo la serikali katika kuifanya Tanzania kuwa ya Kijani.

Kamishna Nshare ameyasema hayo Aprili 8,2024 wakati akizungumza na maofisa wa Ofisi wa Makamu wa Rais walipomtembelea ofisini kwake wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wa Taifa 2024 wilayani Same.

Amesema katika Wilaya ya Same mabadiliko ya tabianchi yameleta athari kubwa ya ukame wa muda mrefu na upepo mkali kwa wananchi kwenye baadhi ya maeneo.

“Wilaya kupitia TFS imeendelea na zoezi la uhamasishaji upandaji miti kwenye maeneo ya vyanzo vya maji pamoja na makazi ili kukabiliana na changamoto hii.

“Kitalu cha miche ya miti cha hapa ni miongoni mwa vitalu 11 vilivyopo TFS Kanda ya Kaskazini na tangu ianzishwe mwaka 2017/18 miti ya aina mbalimbali imepandwa takribani 80,000.

TFS kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza agizo la serikali la kupanda miti 1,500,000 kila mwaka kupitia kampeni ya ‘Fanya Same ya Kijjani.

Kamishna Nshare ameongeza kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2023/24 imefanikiwa kupanda miti zaidi ya milioni 10 sawa na 73% ya lengo la kupanda miti 13,500,000.

Kwa upande wake Afisa Misitu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Thimotheo Mande ameipongeza TFS kwa kusimamia sheria ndogo ya uhifadhi wa mazingira.

“Tuzidi kushirikiana katika kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa miti kwa jamii ili kujua umuhimu wa kutunza miti.

“TFS izidi kushirikiana na kamati za mazingira za kata na vijiji kwa ajili ya kusimamia miti yote inayopandwa katika ngazi za kata na vijiji,” amesema Bw. Mande.

Jamii imeaswa kupanda miti inayostahimili ukame na hali ngumu hasa katika maeneo tambarare ya Wilaya ya Same.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge Kitaifa 2024 inasema “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu.”

Settings