JKT waendelea kutekeleza maelekezo ya kutumia nishati safi ya kupikia

Apr, 14 2024

Kambi ya Maramba ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) imeanza kutekeleza katazo la Serikali la matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambapo ilielekezwa hadi kufikia Januari 31,2024 taasisi zote zinazolisha watu kuanzia 100 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Kaimu Kamanda Kikosi cha Maramba JKT Meja Lino Mambosho amesema hayo Aprili 13,2024 utekelezaji wa maelekezo hayo kwa vitendo umeanza muda mrefu kwa kutumia gesi pamoja na umeme katika majiko yao.

Amesema kuna faida kubwa wanaiona katika matumizi ya nishati safi japo kutokana na mazingira yao gharama ya gesi ni kubwa kulinganisha na kuni.

“Vijana wanatumia gesi pamoja na umeme katika upishi wa chakula na hapa tunafundisha kutengeneza mikate lakini bado wanatumia gesi na umeme hivyo mkaa ni mara chache pale inapotubidi kufanya hivyo,” amesema Maj. Mambosho.

Afisa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Anthony Migeka amesema imekuwa faraja kuona taasisi kubwa kama JKT Maramba wanafuata katazo la Serikali.

“Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii kuendelea kutunza mazingira na taasisi kubwa kama shule, vyuo na makambi kutumia nishati safi kwa faida yetu sote katika kutunza mazingira.”

Afisa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Bw. Mamboya Buge amesema katika Halmashauri ya Mkinga Maramba JKT imekuwa mfano kwani ndio taasisi ya kwanza kutumia Nishati Safi.

Amesema ataangalia namna ya kuonana na uongozi ili kujifunza kutoka kwao namna walivyofanikiwa kuhama kwenye matumizi ya kuni na mkaa hadi kufikia kwenye Nishati Safi ya kupikia.

Lengo la Serikali ni kudhibiti uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti kwa kiwango kikubwa na kulinda afya za wananchi, katazo la matumizi ya kuni na mkaa linazihusu taasisi zote za umma na za binafsi Tanzania Bara.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge Kitaifa 2024 inasema “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu.”

Settings