Dkt. Jafo: Watanzania tuuenzi Muungano wetu

Apr, 08 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Watanzania wana kila sababu ya kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amewataka Watanzania kutembea kifua mbele kujivunia Muungano huo adhimu ambao umeleta faida lukuki zikiwemo uhusiano mzuri baina ya wananchi wa pande zote mbili katika Nyanja mbalimbali.

Dkt. Jafo amesema hayo wakati akizungumza kwenya uzinduzi wa Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa jijini Dodoma leo Aprili 08, 2024.

Waziri Dkt. Jafo amewashukuru na kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa usimamizi wao na kuwezesha utatuzi wa changamoto 15 kati ya 18 ndani ya miaka mitatu ya uongozi wao.

“Leo hii tunaanza mbio za miaka 60 ya Muungano na hili ni jambo la kipekee tangu Muungano ulipoundwa, mwaka huu nchi yetu inatengeneza historia yake ya kipekee na sisi Ofisi ya Makamu wa Rais yale yote ambayo Watanzania walipaswa kujivunia tumejitahidi kufanya kila linalowezekana,” amesema Dkt. Jafo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma amesema kuwa Muungano ni tunu kubwa hivyo ni wajibu weu kuulinda na kuutunza.

Amesema Watanzania hawana budi kuutetea kwa hali yoyote ile kuhakikisha unaendelea kudumu ili wananchi waishi kwa usalama na Amani.

Mhe. Hamza amewataka Watanzania kuwaenzi Waasisi wa Muungano Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambaye Aprili 07, 2024 ilikuwa kumbukizi ya miaka 52 ya kifo chake.

Halikadhalika Mhe. Waziri Hamza amesema kuwa uzinduzi rasmi wa sherehe za Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar unatarajiwa kufanyika Aprili 14.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kuratibu Muungano katika utulivu na amani na kufanya nchi hizi mbili zikiendelea kuimarika kwa mshikamano mkubwa

Pia, amewapongeza viongozi wakuu kwa kuendeleza Muungano ambao una historia ya muda mrefu na kuendelea kuimarisha na kuufanya muungano kuendelea kuwa imara.

Kilele cha Sherehe za Miaka 60 ya Muungano kinatarajiwa kufanyika Aprili 26, 2024 ambapo kitatanguliwa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika Tanzania Bara na Zanzibar.

Kaulimbiu ya sherehe za mwaka 2024 ni ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa letu’

Settings