Dkt. Jafo: Ni jukumu la kila mmoja kulinda miti anayopanda ili istawi

May, 03 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha analinda miti anayopanda na kuitunza ili istawi na kufanya taifa kuwa la kijani hivyo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo aliposhiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ulipotembelea na kukagua mradi wa kiwanda cha mkaa mbadala kinachojengwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo tarehe 03 Mei, 2024.

Dkt. Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe amesema Kiwanda hicho kitakapokamilika kitasaidia katika utunzaji mazingira kwakuwa jamii itaachana na kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa na kuanza kutumia mkaa mbadala rafiki wa mazingira.

“Niwapongeze STAMICO kwa kuwa mradi huu utaleta heshima kubwa katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambayo ndio kilio chetu, tuendelee kuyalinda na kuyatunza.

“Mradi huu utakwenda kuokoa zaidi ya hekta milioni nne zinazopotea kutokana na vitendo vya ukataji miti kwa sababu za shughuli mbalimbali za kibinadamu tunazozifanya kila siku,” amesema Dkt. Jafo.

Halikadhalika Dkt. Jafo amesisitiza kwamba kibali cha ujenzi kiambatane na upandaji wa miti isiyopungua mitatu.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Bw. Godfrey Mnzava amesema juhudi katika Kampeni ya Soma na Mti isimamiwe vyema ili wanafunzi wawe wazalendo katika utunzaji wa mazingira.

Amesema wanafunzi wanapopewa elimu vizuri ya kulinda na kutunza mazingira itasaidia kwa kuwa wataisambaza nyumbani kwao na kutoa elimu kwa wengine.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Bw. Deus Magala amesema mradi unalenga kuchangia juhudi za kitafa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uharibifu wa mazingira na ukataji miti ovyo kwa kuzalisha nishati mbadala.

Ameongeza katika juhudi za matumizi ya nishati mbadala mkaa huo utauzwa kwa bei nafuu kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia.

Settings