Dkt. Jafo azielekeza halmashauri kupanda miti pembeni ya barabara

Mar, 28 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amezielekeza halmashauri zote Tanzania Bara kupanda miti pembezoni mwa barabara ili kuipendezesha miji na kuhifadhi mazingira.

Dkt. Jafo ametoa maelekezo hayo wakati akizindua ‘Mradi wa Twiga wa Kijani’ unaohusisha zoezi la upandaji wa miti katika shule za 60 za mikoa sita ya Tanzania, leo Machi 28, 2024 katika viwanja vya Shule ya Msingi Jeshini, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Amelipongeza Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuliwezesha Shirika lisilo kiserikali la WBM kwa kuandaa mradi huo na zoezi la upandaji wa miti aliloliongoza akisema kuwa litasaidia kuwajengea wanafunzi ari ya kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikitembelewa na wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani hususan baada ya kuzalishwa kwa filamu ya ‘Royal Tour‘ na Serikali kununua ndege nyingi zaidi hivyo ni muhimu tukatengeneza madhari ya kuvutia pembezoni mwa barabara kwa kupanda miti.

Waziri Dkt. Jafo ameyataka majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeya, Arusha na Dodoma kuwa ya mfano wa kuigwa katika kutekeleza maelekezo ya kupandwa miti pembezoni mwa barabara.

Halikadhalika, amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri za manispaa kusimamia zoezi la usafi katika maeneo yao kwa kuwa na wakandarasi wa usafi wenye vifaa bora.

“Haipendezi hata kidogo unafika katika jiji fulani au manispaa fulani uchafu umetapakaa katika mitaro mvua ikinyesha mitaro inaziba na wakati mwingine malori yameegeshwa wakandarasi hawajatoa taka, nielekeze tena mtekeleze maelekezo hayo, imani yetu halmashauri zetu zitakuwa safi,“ amesisitiza.

Ametumia nafasi hiyo pia kuzisihi kampuni za nishati safi ya kupikia kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na kuni na mkaa ili kuokoa miti inayokatwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Sengerema Asenyi Ngaga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, amesema kwa kutokana na idadi kubwa ya watu katika mkoa huo suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu.

Amesema endapo mazingira yasipotunzwa kutahatarsisha Maisha hivyo hawana budi kuunga mkono juhudi za Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla katika kupanda miti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania Mhandisi Ladislaus Matindi amesema kuwa usafiri wa anga unaweza kuchangia ongezeko la joto duniani kwa asilimia tano.

Amesema kutokana na hali hiyo Jumuia ya Usafiri wa Anga wamekubaliana kutumia injini zisizotumia mafuta ya petroli na badala yake itumike nishati mbadala ya mafuta ya nafaka za mbegu jamii ya maharage.

Pia, Bw. Matindi amesema zinachukua hatua ya kuhakikisha ndege hazichangii katika kutoa gesi chafu angani pamoja na kupunguza muda wa kukaa angani kwa ndege hizo ili kupunguza gesijoto inayotoka.

Mkurugenzi wa WBM Bi. Latifa Mohamed amesema lengo la mradi ni miti 6,000 katika kupandwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwenye shule sita za msingi na sekondari katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara.

Bi. Latifa amesema kupitia mradi huo wenye kaulimbiu ‘Mazingira yetu, Maisha yetu‘ utasaidia kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira kwa kutoa elimu ya mazingira kwa wanafunzi

Settings