Dkt. Jafo apongeza uimara wa EAC katika kulinda mazingira

Nov, 23 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amepongeza wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano huo hatua inayosaidia kuimarisha Maisha ya wananchi wa ukanda huo hususan kuhifadhi mazingira.

Ametoa pongezi huo aliposhiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaojadili masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Usalama wa Chakula uliotanguliwa na Mkutano wa Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Usalama wa Chakula, Ngurduto mkoani Arusha Novemba 23, 2023.

Amesema kama nchi tunajivunia kuwa na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha uhusiano mzuri na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla.

“Tunashukuru tupo hapa Arusha tunakutana mawaziri na viongozi wakuu wa mataifa haya hivyo, mkutano huu ni muhimu sana kwa kuwa unahusisha ajenda muhimu ya mazingira na ambayo ni muhimu kwa usalama wa chakula,” amesema Dkt. Jafo.

Mkutano huo unajadili mada mbalimbali zikiwemo Maazimio ya Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Nairobi na uwiano wa athari zake kwa eneo la Jumuiya; Maazimio ya Mkutano wa Mifumo ya Usalama wa Chakula Kuhakikisha Usalama wa Chakula kupitia mikakati na mbinu mbalimbali za kurekebisha na Kuonesha Mafanikio ya Kilimo cha kisasa, kinachotokana na matumizi ya teknolojia na mbinu mbalimbali za ubunifu katika eneo hilo.

Mkutano huo wa Majadiliano ya Juu unatarajiwa kutoa na msimamo wa pamoja wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuelekea Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika Dubai kuanzia Novemba 28, 2023.

Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Kuongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi kwa usalama wa chakula na mazingira endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki".

Settings