ZIARA YA MAKAMU WA RAIS WILAYANI SAME NA MWANGA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema hakuna Maendeleo pasipo Utawala bora.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro.

“Viongozi wa Halmashauri, Viongozi wa Wilaya wasipokuwa na Utawala bora, wasiposhirikiana, Chama, Serikali, Wilaya, Halmashauri tusitegemee kuwa na maendeleo tutalalamika siku zote” alisema Makamu wa Rais.

Leo katika ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za kimaendeleo Makamu wa Rais alitembelea miradi mbali mbali katika Wilaya ya Same na Mwanga.

Akiwa Wilayani Same, Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya New Dawn, Shule ambayo itakuwa ya mchepuo wa masomo ya sayansi na ni maalum kwa Watoto wenye mahitaji maalum na Yatima pamoja na kuweka jiwe la msingi la uzinduzi wa ofisi za Wakala wa Misitu Wilaya ya Same.

Makamu wa Rais amewahimiza Wakala wa Misitu nchi kuwapa wananchi miche ya kutosha na kuimarisha ulinzi katika hifadhi ya misitu.

Akiwa Wilayani Mwanga, Makamu wa Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe ambao awamu ya kwanza imekamilika kwa asilimia 76%.

Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amesema kwa sasa awamu ya kwanza ambayo ni Miundombinu ya mradi huo imekamilika kwa asilimia 76% na umegharimu bilioni 94.65 ambapo awamu ya pili itakuwa usambazaji wa maji Same na awamu ya tatu itakuwa usambazaji wa maji Mwanga.

“Serikali imejipanga kila eneo ambalo maji yanapita wananchi watafaidika na maji hayo” alisema Waziri wa Maji.

Kwa upande wake Makamu wa Rais alisema Serikali imedhamiria kutatua tatizo la maji nchi na kuwataka wananchi kutambua kuwa miradi hii ya maji ina gharama kubwa hivyo inabidi wawe walinzi wazuri wa miundombinu ya maji.

Katika ziara hiyo Wilayani Same na Mwanga Makamu wa Rais ameongozana na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Wiliam Lukuvi.