ZIARA YA MAKAMU WA RAIS – IKUNGI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza kwa asilimia kubwa mambo yaliohaidiwa kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji utakaohudumia wakazi zaidi ya 2600 wa kijiji cha Ulyampiti, wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

Ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Singida, Makamu wa Rais ametoa agizo kwa Wizara ya Maji kuhakikisha katika mpango wa visima 20 wilayani Ikungi kimoja kichimbwe kijiji cha Mang’onyi. Pamoja na mambo mengine Makamu wa Rais alitembelea zahanati ya Mang’onyi na kituo cha afya cha Ihanja na kujionea maboresho mbali mbali ikiwa pamoja na kufungwa mashine mpya ya upasuaji.

Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ihanja Madukani Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa bima ya afya kwa wananchi hao ikiwa na kuzitaka mamlaka husika kutoa elimu ya kutosha ili kila mwananchi aelewe mpango wa Serikali wa Bima kwa wote.

Aidha Makamu wa Rais amewataka wakazi wa Ihanja kutoruhusu mimba za utotoni kwani zinawanyima fursa ya mabinti wao kuja kuwa viongozi na wataalam wa badae, pia aliwasihi wananchi kuacha kukeketa mabinti kwani ukeketaji una athari nyingi zikiwemo vifo wakati wa kujifungua. 

Makamu wa Rais amechangia mabati 200 kuunga mkono juhudi za Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi. Wakati huohuo Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe. Elibariki Kingu amesema Chama na Serikali ni kitu kimoja kwani wanashirikiana katika kila jambo la kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa.