Waziri Zungu, Dkt.Kalemani wakagua athari za mazingira Mtera na Kidatu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani wametembelea vituo vya kufua umeme kwa maji ya mabwawa ya Mtera na Kidatu kukagua hali ya maji na athari za mazingira zinazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Kufuatia hali hiyo wizara hizo mbili kwa pamoja zimeunda Kamati ya wataalamu mbalimbali kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kuhifadhi maji kwenye bwawa hata baada ya kipindi cha mvua.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Zungu alisema lengo la kuundwa kwa Kamati hiyo ni kulinda mabwawa pamoja na uoto wa asili usipotee na kuwa lazima maji ya kuzalisha umeme yapatikane kutoka kwenye vyanzo vya maji.

Aliongeza kuwa pamoja na hayo pia wananchi washirikishwe katika utunzaji wa vyanzo vya maji kwani nchi inategemea umeme kujiendesha hasa tunapoelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda na umeme wa maji ndio wa bei nafuu.

Aidha, waziri huyo alilitaka Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira kukutana ili kutoa tathmini ya uharibifu uliotokea katika kipindi ambacho maji yamefunguliwa katika mabwawa hayo.

Kwa upande wake Waziri Kalemani alisema kuwa uhifadhi wa maji utaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na hivyo ni kuna umuhimu wa kuangalia namna bora ya kuwaelimisha wananchi wanaofanya shughuli za kijamii pembezoni mwa mabwawa ya kufua umeme.

Alibainisha kuwa Wizara ya Nishati ina wajibika katika kulinda na kutunza miundombinu yote ya uzalishaji wa umeme na hivyo wanashirikiana na NEMC ili kuulinda Mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere.