WAZIRIWaziri Zungu afanya ziara Ilala kutatua changamoto za uchafuzi wa mazingira wa mifereji ya maji ya mvua

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amefanya ziara katika Mtaa wa Sharif Shamba Ilala Jijini Dar es Salaam kukagua mfereji wa maji ya mvua katika eneo hilo kwa lengo la kuangalia ubora wa mfereji huo.
Mhe. Zungu akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Benjamin Mchwampaka pamoja na wataalamu wa mazingira amesema kuwa baada ya ujenzi kukamilika kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu changamoto zilianza kujitokeza jambo ambalo lilileta wasiwasi kwa Wananchi.
 “Nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu mfereji huu kuwa kuta zake zimeanza kubomoka, imenilazimu kuwaita wataalamu wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kitengo cha mazingira, wataalamu kutoka NEMC na Mkandarasi aliyepewa tenda hii. Bahati nzuri mkandarasi amekubali kuukarabati tena mfereji huu.” amesema Mhe. Zungu
Waziri Zungu pia amewataka viongozi mbalimbali wa mtaa kuhakikisha wanafanya doria mara kwa mara ili kuzuia wahalifu wanaochafua mfereji huo.
“Wakuu wa kamati za ulinzi na usalama wa mtaa, na wakuu wa kamati za mazingira za mtaa ni lazima mfanye doria za mara kwa mara kuhahakisha mifereji hii haichafuliwi kwa takataka ili wananchi waishi salama na Amani katika maeneo yao.” ameongeza Mhe. Zungu
Kwa upande wake mwenyekiti wa Mtaa wa Sharif Shamba Omary Mkumbi amesema kuwa mfereji huo umekua na changamoto ikiwemo uchafuzi wa mazingira unaofanywa kinyemela na wananchi.
“Mfereji wetu hauna maelekezo ya kusafishwa mara kwa mara. Wako wananchi wanaochafua mfereji huu, tunaweka mtego lakini bado hatujawabaini wahusika wanaotenda vitendo hivyo. Lakini kamati yangu ya mazingira inajitahidi lakini binadamu ni wazito yaani saa sita usiku, saa saba ndio wanakuja kumwaga uchafu.” Amesema Mkumbi
Nae kaimu Mkurugenzi mkuu wa NEMC Benjamin Mchwampaka ametoa rai wahusika wa  mfereji huo kutafuta mbinu mbadala ya kuulinda kutokana na kuwa na umuhimu mkubwa kwa usalama wa maeneo hayo.
“Changamoto tunayoiona kama NEMC ni hali ya utupaji wa takataka kwenye mfereji na kutiririsha maji machafu. Kwa mujibu wa sheria ya mazingira maji machafu hayatakiwi kutiririshwa kwenye mfereji wa maji ya mvua. Sisi tunatoa rai pande zote mbili za mfereji  watunze mfereji huu ambao ni muhimu sana kwa Wananchi wa maeneo haya.” amesema Mchwampaka
Mfereji huo wa maji ya mvua umejengwa kwa ushirikiano wa umoja wa mataifa na ofisi ya Makamu wa Rais na umekuwa msaada mkubwa katika kuzuia mafuriko licha ya kuwepo kwa changamoto za uchafuzi wa mazingira zinazofanywa na Wananchi wa eneo hilo.