Waziri Makamba awahakikishia wananchi upatikanaji wa uhakika wa mifuko mbadala

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe January Makamba amewahakikishia wananchi kuwa upatikanaji wa mifuko mbadala utakuwa wa uhakika.

Mhe. Makamba ametoa kauli hiyo leo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya katazo la mifuko ya plastiki litakaloanza kutekelezwa Juni mosi, 2019.

Alisema kuwa wapo wawekezaji ambao tayari wameonesha nia ya kuzalisha mifuko mbadala ya karatasi ambapo uzalishaji huo utasaidia kukuza uchumi.

Waziri Makamba alibainisha kuwa hapa nchi kuna malighafi za kutosha kuweza kutumika katika uzalishaji wa bidhaa hizo hata kufikia hatua ya kusafirishwa nchi jirani.

Pia aliongeza kwa kusema kuwa matumizi ya mifuko mbadala isiyokuwa ya plastiki yanawezekana kama wote tutazungumza kwa sauti moja  na kubadilika kifikra.

“Watanzania zamani tulikuwa tukienda sokoni kununua vitu tunabeba vikapu lakini siku hizi nashangaa tunakwenda mikono mitupu tukitegemea tupewe mifuko, sasa tubadilike,” alisisitiza.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. George Simbachawene alipongeza hatua hiyo ya Serikali ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki.

Mhe. Simbachawene alisema kuwa katazo hilo la mifuko ya plastiki litachochea katika kuongeza ajira kwa wananchi wenye ujuzi wa usukaji wa mifuko kama vile vikapu.

Alitaka kampeni hiyo iungwe mkono na ifanyike katika mikoa yote ya Tanzania ili wananchi wapate elimu kuhusu athari za mifuko hiyo sambamba na fursa za mifuko mbadala.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe January Makamba akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.