WAZALISHAJI MIFUKO MBADALA WAHAKIKISHA SOKO LA UHAKIKA

Wazalishaji wa Mifuko Mbadala wamesema wamejipanga kukidhi mahitaji ya soko popote nchini na kwa muda muafaka wakati ambapo Serikali imepiga mifuko ya plastiki kuanzia Juni mosi mwaka huu.

Wamesema mifuko mbadala inayozingatia utunzaji wa mazingira ipo ya aina nyingi na wanatarajia kuwa itakuwepo ya kutosha kuendana na pia na ukuaji wa uchumi.

Wametoa kauli hiyo katika taarifa yao kwa umma ambapo wamesema tangu Serikali ilipotangaza katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki wazalishaji wa mifuko mbadala walianza kuona fursa na kuanza kuzalisha mifuko hiyo.

Waliongeza kuwa baada ya katazo hilo wazalishaji wa mifuko mbadala wameongeza kasi ya uzalishaji na tayari wameagiza mashine kwa ajili ya kuanza uzalishaji huo.

Aidha, walibainisha kuwa wazalishaji wa mifuko mbadala wameanza kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali na tunawaomba watanzania kuona fursa ya mifuko hiyo ikiwa ni sehemu ya kujitengenezea kipato.

“Tunawahakikishia wananchi na wadau mbalimbali wanaotaka kuwekeza kwenye fursa hii kuwa malighafi inapatikana sehemu mbalimbali nchini kwa mfano karatasi inapatikana Mufindi Paper Mills Ltd na Tanpack Tissues Ltd.

“Malighafi ya vitambaa laini inapatikana Harsho Group mjini Moshi, mikeka, katani na pamba vinapatikana maeneo mbalimbali nchini pia vitambaa vya nguo vinapatikana madukani na soko kuu la Kariakoo,” walisisitiza.

Walitoa mwito kwa Watanzania kuona fursa ya mifuko mbadala kuwa ni sehemu ya kujitengenezea kipato kwani wazalishaji wameanza kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali.

Walishauri Serikali na taasisi husika kutoa mafunzo na teknolojia ya kutengeza mifuko mbadala na kuwa halmashauri zielekeze misaada na mikopo kwa vikundi au watu wanaoingia kwenye uchumi huu mpya wa mifuko hiyo.

Walizishauri Serikali za Mikoa na Halmashauri mbalimbali kuelekeza nguvu zao kukuza uchumi wa wananchi wao kwa kuwekeza kwenye mifuko mbadala na kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa upungufu utakaojitokeza sambamba na kuchochea uchumi na kuacha mazingira salama.

Katazo la mifuko ya plastiki lilitangazwa Aprili 10, 2019 lilitangazwa bungeni na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na linasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ikishirikiana na kikosi kazi kutoka taasisi mbalimbali.