WADAU WA MAZINGIRA WAHIMIZA MATUMIZI YA MIFUKO MBADALA WA PLASTIKI

Imebainika kuwa Mto Nile, ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria, ni mto wa tano miongoni mwa mito kumi duniani iliyoorodheshwa kwa kusafirisha kiwango kikubwa cha taka za plastiki kwenda baharini kutoa nchi kavu ikiwa ni takriban tani 85,000 kwa mwaka kwa mujibu wa tafiti za Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira.

Akifungua kikao cha siku moja cha wadau kujadili fursa zilizopo katika uzalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki Jijini Mwanza, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Balozi Joseph Sokoine amesema kuwa Takwimu zinaonesha kuwa takriban nusu ya taka za plastiki zinazozalishwa zinajumuisha vifungashio na mifuko ya plastiki.

Balozi Sokoine amesema kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira linakadiria kuwa hali ya sasa ya uzalishaji na matumizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki ikiendelea, ifikapo mwaka 2050 takataka za plastiki zitakuwa nyingi kuliko samaki baharini, na kusisitiza kuwa changamoto za taka za plastiki si suala la afya ya jamii na hifadhi ya mazingira tu bali linagusa uchumi na mustakabali wa maisha yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo.

“Uchafuzi wa taka za plastiki baharini ni changamoto ya Dunia inayohitaji hatua za haraka. Hivyo, ni muhimu kama Taifa tukashirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuchukua hatua madhubuti ili kuinusuru Dunia dhidi ya janga hili” Balozi Sokoine alisisitiza.

Kwa upande mwingine Afisa Mazingira kutoka Mkoa wa Mwanza Bw. Mangabe Mnilago amesema ni vema jamii ikafahamu kuwa uzalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki ni fursa kwa wananchi na kuwasihi kuwekeza katika sekta hiyo.

Serikali kwa muda sasa imekuwa ikifanyia kazi suala la kuzuia uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ya kubebea bidhaa nchini. Dhamira ambayo inafanyiwa kazi na kikao cha leo ni moja ya hatua za kimkakati katika kufikia azma hiyo.

Kikao cha leo kimelenga kupata mwelekeo wa hatua muafaka ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaochangiwa na mifuko ya plastiki ikiwa ni moja ya hatua za kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala iliyo rafiki kwa mazingira inayotengenezwa kwa karatasi, vitambaa vya nguo na hata vikapu vya asili na kimejumuisha wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa za karatasi na plastiki, wawakilishi wa sekta binafsi, baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali na kimefanyika Katika Ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu Mwanza.