Tanzania kushiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi Scotland

Tanzania inatarajiwa kushiriki Mkutano mkuu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (COP 26) utakaoandaliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Uingereza na Italia ambao utakafanyika mjini Glasgow, Scotland.

Hayo yamebainika leo wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Sarah Cook aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho pamoja na kuzungumza kuhusu ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili Waziri Zungu akifafanua alisema kuwa Mkutano huo Tanzania itatoa mchango wake wa namna inavyopambana na changamoto hii ya kimazingira.

“Tumezungumza hasa uhusiano mzuri tulionao na nchi hiyo lakini pia kuhusu mkutano utakaofanyika Glasgow na tunatakiwa tutoe vipaumbele vyetu vya namna Tanzania itasaidiaje kuokoa mazingira kiulimwengu, namna gani inadhibiti hewa ya ukaa isizagea katika maeneo mengine,” alisema.

Waziri Zungu alibainisha kuwa watalamu wanakaa kwa ajili ya na kushughulikia vipaumbele kuhusu hatua za kuchukua katika mabadiliko ya tabianchi ili vipitishwe na mamlaka zinazohusika kabla ya kuwasilishwa kwenye mkutano huo.

Kwa upande wake Balozi Cook aliipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa hatua zake katika kupambana na uharibifu wa mazingira pamoja na changamoto zilizopo.

Alisema kuwa mkutano huo utasaidia nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ambazo zinaathirika na mabadiliko ya tabianchi kuwa na fursa ya kupata misaada ya  kifedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Kiukweli mabadiko ya tabianchi yanaathiri sana wananchi hasa wakulima wanashindwa kuwa na kilimo cha ukakika kwani hali ya hewa haitabiliki hivyo tumejipanga kutoa elimu ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema.