TAMKO LA WAZIRI WA NCHI (MUUNGANO NA MAZINGIRA) – SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

TAMKO LA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA LA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 5 JUNI, 2019

 Ndugu wananchi,

Tarehe 5 Juni, 2019 watanzania tunaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yaliamuliwa mwaka 1972, katika mji wa Stockholme nchini Sweden, kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira. Katika mkutano huo, Jumuiya ya Kimataifa iliazimia tarehe 5 Juni, kila mwaka iwe ni kilele cha maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani.

Ndugu wananchi,

Madhumuni ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuelimisha jamii, masuala mabalimbali yahusuyo Mazingira na pia kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maadhimisho haya. Aidha, jamii zinahamasishwa  kuwa mstari wa mbele  kuchukua hatua za makusudi za kuhifadhi na kulinda mazingira ya maeneo yao kwa maendeleo endelevu. Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa jamii mbalimbali kufahamu wajibu wao wa kuzuia madhara na mabadiliko hasi ya Mazingira yanayotokana na shughuli za kijamii na kuhamasisha jamii kufanya mazingira yao kuwa salama na safi ili kila mtu afurahie hali hiyo katika maisha ya sasa na ya vizazi vyinavyokuja.

 Ndugu wananchi,

Kimataifa maadhimisho haya yanafanyika katika mji wa Hangzhou nchini China na kaulimbiu ya Kimataifa inayoongoza maadhimisho haya ni “Uchafuzi wa Hewa” (Air Pollution). Kaulimbiu hii inahimiza jamii kuepuka shughuli zinazo sababisha uchafuzi wa hewa. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho haya China ni kutokana na nchi ya China kuwa na viwanda vingi ambavyo uzalishaji wake unasabisha uchafuzi wa Hewa. Hivyo, maadhimisho haya yanatoa fursa kwa nchi ya China na nchi nyingine duniani kuhamasika kuepuka shughuli zinazosababisha uchafuzi wa mazingira na kuwaepusha watu wake na maradhi yatokanayo na uchafuzi wa hewa.

Ndugu Wananchi,

Mwaka huu hapa nchini hatutakuwa na maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani  na badala yake kila Mkoa utafanya shughuli za maadhimisho katika maeneo yake kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho haya isemayo: “Tumia mifuko mbadala wa Plastiki; kwa ustawi wa Afya, Mazingira na Maendeleo ya Uchumi”. Kaulimbiu hii ni mwitikio wa Taifa wa Tamko la Serikali la kukataza uzalishaji, uingizaji ndani ya nchi usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki na kuhimiza wananchi kutumia mifuko mbadala. Tamko hili limetokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na utupaji ovyo wa mifuko ya plastiki ambayo imeleta madhara makubwa ya kimazingira, afya za viumbe hai, ikiwemo binadamu wanyama, pamoja na kuathiri uchumi  wa nchi kwa ujumla. Aidha, mifuko ya plastiki imekuwa sehemu muhimu ya jamii yetu, lakini changamoto ya usimamizi na athari za taka za plastiki nchini na duniani inahatarisha mustakabali wa ustawi wa jamii, uchumi na mazingira kwa kuwa mifuko hii huchukua muda wa takriban miaka 500 kuoza.

Ndugu Wananchi,

Hapa nchini, uchafuzi  utokanao wa mifuko ya plastiki unaathiri sana mazingira ya mito mabwawa, maziwa, na bahari ambako viumbe waishio katika mazingira hayo wako hatarini kutoweka. Aidha, uchafuzi utokanao na mifuko ya plastiki umesababisha kuziba kwa miundombinu ya maji ya mvua na majitaka hasa katika maeneo mengi ya miji yetu katika kipindi cha masika na kuchangia kuenea kwa magonjwa ikiwemo kipindupindu, dengue, uharibifu wa mali na hata vifo vya mifugo na binadamu.

Ndugu Wananchi,

Azma ya kukomesha matumizi ya mifuko ya plastiki ni ya dunia nzima. Kwa kutambua hilo, Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira ambalo ndiyo muhimili mkuu wa usimamizi wa mazingira kimataifa, mwaka 2014 liliazimia kuwa uchafuzi wa mazingira unaochangiwa na taka za plastiki unahitaji hatua za haraka za kukomeshwa. Hadi sasa, zaidi ya nchi 100 duniani zikiwemo nchi 25 kutoka Bara la Afrika zimechukua hatua mbalimbali kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki. Aidha, mtakumbuka kwamba kuanzia mwezi Mei mwaka huu serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira imekuwa ikihamasisha jamii kupitia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuacha kutumia mifuko ya plastiki na kutumia mifuko mbadala.

Ndugu wananchi,

Kwa muktadha huu, shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira  hapa nchini mwaka huu pamoja na mambo mengine, zilenge kuhamasisha jamii kutumia mifuko mbadala wa plastiki na kuacha kuzalisha, kusambaza, kuingiza na kutumia mifuko ya plastiki, kufanya usafi wa maeneo mbalimbali na kukusanya taka zote za mifuko  na kuzitupa kwenye madampo yaliyobainishwa.

Kwa kutambua changamoto za mifuko ya plastiki na kuzingatia mwelekeo wa kimataifa, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendesha warsha za wadau mbalimbali ili kuhamasisha uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya mifuko mbadala wa plastiki. Hadi sasa hapa Tanzania kuna viwanda 27 vinavyozalisha mifuko mbadala wa plastiki. Nachukua fursa hii kuhamasisha jamii ya watanzania kuwekeza kwenye teknolojia ya uzalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki ili kuweza kulinda mazingira, afya pamoja na kustawisha hali ya uchumi binafsi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

 Ndugu wananchi,

Ni muhimu ikaeleweka kuwa tuliishi kwa muda mrefu bila mifuko ya plastiki na maisha yaliwezekana. Baadhi ya nchi za jirani ambazo zimeshapiga marufuku mifuko hii zinadhihirisha ukweli huu. Aidha, hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki itaibua fursa mpya za ajira na kipato kwa viwanda, vikundi vidogo vidogo na wajasiriamali katika uzalishaji wa vikapu vya asili na mifuko mbadala ya karatasi, nguo, katani na mingineyo.

 Ndugu wananchi,

Natoa wito kwa Mikoa yote kushirii kikamilifu katika maadhimisho haya kwenye mikoa yenu kwa kuhamasishana na kelimishana masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira husasan kutumia mifuko mbadala wa plastiki. Aidha, nawahamasisha wananchi wote kushiriki shughuli zote za maadhimisho hususan kuendelea kukusanya mifuko ya plastiki kutoka kwenye maeneo yote ilipo kama vile majumbani, maofisini, madukani, sokoni, mashuleni, vyuoni na ile inayozagaa kwenye maeneo mbalimbali na kuipeleka kwenye maeneo yaliyobainishwa ili iweze kufanyiwa utaratibu wa kuiteketeza.

Ndugu Wananchi,

Mwisho, napenda kuvipongeza vyombo vya habari, wadau mbalimbali wa Mazingira kama vile UNEP, WWF, na wengine kwa kushirikiana na serikali kuhamasisha jamii kutokomeza mifuko ya plastiki.

Nimalizie kwa kusisitiza kwamba, sote tuna jukumu la kuanza kubadilika kutoka kwenye matumizi ya mifuko ya plastiki na kuanza kutumia mifuko mbadala wa plastiki. Tukumbuke kwamba suala la hifadhi ya mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo.

January Y. Makamba (MB)

Waziri wa Nchi OMR-Muungano na Mazingira