TAARIFA KWA UMMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

TAARIFA KWA UMMA

Ofisi ya Makamu wa Rais ilianza kutekeleza azimio la Serikali la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia tarehe 1 Juni 2019. Tunashukuru umma wa Watanzania kwa kuitikia vyema utekelezaji wa katazo hili.

Hata hivyo, kumeanza kujitokeza uvunjifu wa sheria katika uzalishaji na uingizaji wa mifuko mbadala aina ya non-woven. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeweka vigezo vya mifuko mbadala aina ya non-woven inayoweza kutumika nchini. Vigezo hivyo ni pamoja na:

  1. Uzito usiopungua GSM 70 (Gram per Square Metre)
  2. Iwe inaweza kurejelezwa (Recyclable)
  3. Ioneshe uwezo wa kubeba (Carrying capacity)
  4. Iwe imethibishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)

Baadhi ya wafanyabishara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza/kuzalisha mifuko mbadala aina ya non-woven ambayo haikidhi vigezo tajwa.

Aidha, kumekuwa na matumizi yasiyokubalika ya mifuko myepesi na laini aina ya “Tubings” kubebea bidhaa. Agizo ni kwamba, mifuko hii inapaswa kutumika kama vifungashio vya bidhaa maalumu na viwe na lakiri (seal) ili kuzuia kuongeza bidhaa nyingine katika kifungashio hicho.

Kwa siku za hivi karibuni mifuko hii laini imekuwa ikitumika kama vibebeo jambo ambalo ni kosa kisheria. Hatua ya kuongezeka kwa matumizi yasiyo sahihi ya mifuko tajwa inaanza kuleta athari katika mazingira.

Kikosi Kazi cha Taifa cha kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Kamati za Mikoa/Wilaya wataendesha operesheni kabambe nchi nzima ili kubaini wanaovunja matakwa ya katazo hili ikiwemo watumiaji na wazalishaji wa mifuko mbadala aina ya non-woven isiyokidhi viwango, pamoja na matumizi ya ‘‘tubings’’.

Kumbuka, Mazingira ndiyo yanayolea uchumi wa Taifa letu, hivyo anayeharibu mazingira ni sawa na mhujumu uchumi. Kwa muktadha huo watakaobainika kuvunja Sheria watakachukuliwa hatua stahiki.

Tunaendelea kuushukuru umma wa Watanzania kwa kutekeleza agizo hili na kutunza Mazingira kwa ustawi wa Taifa letu.

Kwa maelezo na ufafanuzi kuhusu suala hili au masuala yoyote yanayohusu mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa namba maalumu za simu kwa ajili hiyo. Mwananchi hataingia gharama kupiga simu katika namba hizi ambazo zinapatikana masaa 24, wasiliana nasi kwa kutuma ujumbe mfupi (SMS) au ujumbe wa Whatsapp kupitia:

KUPIGA BILA MALIPO                                           SMS/WHATSAPP

(0800 110 115)                                                       +255 737 796 253

(0800 110 116)                                                       +255 737 796 252

(0800 110 117)                                                       +255 737 796 249

(0800 110 118)                                                       +255 737 796 250

 

Imetolewa na

Mhandisi Joseph K. Malongo

KATIBU MKUU

04/11/2019