Waziri Zungu aruhusu kutolewa kwa mchanga Bonde la Jangwani

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu ameruhusu kutolewa kwa mchanga uliopo eneo la Msimbazi kwa lengo la kusafisha eneo hilo na kutoa fursa kwa wanamichezo kutumia eneo hilo lililokua likitumiwa kipindi cha nyuma.

“Baada ya ushauri wa wataalam, nimeruhusu mchanga huu utolewe. Watakaokuja kutoa mchanga huu ndio watakaogharamia gharama za kutoa mchanga lakini halmashauri na mamlaka zitapata mapato kupitia tozo mbalimbali.” Amesema Mhe. Zungu

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Benjamin Mchwampaka amesema kuwa NEMC itakuwa ni kati ya mamlaka zitakazofuatilia utendaji wa maelekezo aliyoyatoa Waziri Zungu ili kuhakikisha taratibu na sheria zinafuatwa.

“Maelekezo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Waziri, utaratibu undaliwe, NEMC itakuwepo, Mkurugenzi wa Halmashauri na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa husika tuone namna gani bora vikundi hivyo vitachukua mchanga huu.” amesema Mchwampaka

Nae Mkurugenzi wa manispaa ya Ilala Jumanne Shauri anasema zoezi hilo ni fursa ya kuleta mapato katika Manispaa yake na kumhakikishia Waziri Zungu kuyaelekeza katika maendeleo.

“Sisi Manispaa ya Ilala tumejipanga kukusanya mapato na lengo letu ni kuongeza mapato na hatimaye tuyapeleke kwenye miradi ya maendeleo.” Amesema Shauri huku akiongeza kuwa fedha zitakazokusanywa hapa zitarudi kwenye Manispaa ya Ilala kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Wananchi wa eneo hilo wamefurahishwa na uamuzi wa Waziri Zungu huku wakiangazia zaidi suala la fursa za ujasiriamali pamoja na shughuli za michezo.

“Tunamshukuru sana Waziri wa Mazingira kwa huu ubunifu alioufanya. Hii inafaida kubwa sana ikiwemo kupata mapato kwa vijana wetu. Kwahiyo vile vikundi vitakavyoundwa vitafanya hivyo kama sehemu ya ujasiriamali.” Amesema Lisindo mmoja ya wakazi wa eneo hilo

Mchanga wa eneo la Jangwani umekua kikwazo kwa eneo la Jangwani kutokana na kufunika maneo ya wazi yaliyokuwa yakitumiwa kipindi cha nyuma ikiwemo uwanja wa mpira uliotumiwa na wakongwe mbalimbali wa michezo hapa nchini.