Waziri Zungu afanya ziara kiwanda cha Ocean Alluminium ambacho shehena ya malighafi yake imekwama bandarini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu ametembelea kiwanda cha Ocean Alluminium kilichopo Tabata – Matumbi kinachozalisha Sufuria ili kujionea uendeshwaji wa kiwanda hicho pamoja na kutatua changamoto ya kukwama kwa mzigo wao.

Mhe. Zungu akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt.Samuel Gwamaka pamoja na wataalam mbalimbali wa Serikali, amesema kuwa atakapofanya maamuzi ukaguzi wote stahiki utafanyika.

“Vyombo vya ukaguzi tunavyo na pale tutakapofanya maamuzi hiki wanachokihitaji wamiliki wa kiwanda hiki juu ya mzigo wao huu wa tani 40 hautatoka mpaka wataalam wetu kutoka NEMC pamoja na wataalam wa mionzi kujiridhisha mzigo huu utakuwa ni salama.” Amesema Mhe. Zungu

Akieleza  kilichowapata hadi shehena yao kuzuiliwa Bandarini Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho Arman Arya amesema kuwa waliingiza mzigo huo nchini bila ya kufahamu utaratibu unaopaswa kufuatwa.

“Tuliingiza Kontena la malighafi bila ya kufuata taratibu za hapa nchini. Tulikuwa hatufahamu juu ya taratibu hizo”. Amesema Arya, huku akiongeza kuwa baada ya mzigo wao kuingia nchini ndipo walipofahamu juu ya taratibu hizo na wanamuomba Waziri kama ikiwezekana awasaidie waupate mzigo wao uliokwama Bandarini.

Kutokana na kupokea maombi ya Kiwanda hicho juu ya kupatiwa msaada kutokana na shehena yao ya malighafi kukwama Bandarini, Mhe. Zungu amesema kuwa atashirikiana na vyombo husika kulipatia ufumbuzi suala hilo.

“Tunachukua malalamiko haya ambayo wameyaleta kwangu rasmi maana kwa mujibu wa sheria za Nchi ni Waziri ndiyo mwenye mamlaka ya kushughulikia matatizo na kuhakikisha kama kuna uvunjwaji wa sheria kitu gani kifanywe.” Amesema Mhe. Zungu, huku akiongeza kuwa atashirikiana na Mkurugenzi wa NEMC, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Wanasheria  wa Serikali kutizama namna tatizo hilo linaweza kutatuliwa.

Kwa upande wake Aisha Omary, Meneja Uajiri katika kiwanda hicho anasema kuwa uzalishaji umepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na kukwama kwa malighafi za kiwanda hicho.

“Kiukweli uzalishaji uko chini kutokana na kutokupatikana kwa malighafi lakini tutakapopata malighali za kutosha tunatarajia tutazalisha kwa wingi.” Amesema Aisha

Kiwanda cha Ocean Alluminium Ltd kinazalisha bidhaa za sufuria na soko lake kubwa ni katika masoko ya Jiji la Dar es salaam huku kikiwa na wafanyakazi takriban 100 na kinalipa kodi Serikalini kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 kwa mwaka.