SIKU YA PILI YA ZIARA YA NAIBU WAZIRI – WILAYA YA BAHI

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima ameitaka Kampuni ya Kasco inayojenga kiwanda cha kupasua kokoto katika Kijiji cha Mundemu Wilaya ya Bahi kufika Ofisini kwake ndani ya siku saba kuanzia leo, ili waweze kuelekezwa taratibu za kufuta baada ya kufanya uwekezaji bila kufuata taratibu za kisheria, Ikiwa ni pamoja kuanza kazi za ujenzi bila kushirikisha Wilaya husika na wananchi wa eneo hilo na kutofanya Tathimini ya athari kwa mazingira kwa mujimu wa Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu namba 81(1-5) pamoja na jedwali la tatu

“Kabla ya kuanza uwekezaji huu mkubwa, mwekezaji huyu alipaswa kuwa na cheti cha Tathmini ya athari kwa mazingira, ambao ni muongozo wa namna ya kuendesha shughuli hizo za uzalishaji bila kuathiri mazingira, sisi hatuzuii wawekezaji ila tunataka taratibu zifuatwe” Sima alisisitiza.

Aidha, mwekezaji huyo ametakiwa kuendelea kutekeleza agizo lililotolewa na Uongozi wa Wilaya hiyo la  la kusitisha uendelezaji wa aina yoyoye katika eneo hilo mpaka pale taratibu za kisheria zitakapofuatwa ipasavyo.

Kwa upande mwingine Bw. Gorden Senyegalo Diwani wa Kata ya Mundemu amesema kuwa Mwekezaji huyo wa Kampuni ya Kasco amekiuka makubaliano waliyokubaliana katika Mkutano wa Serikali ya Kijiji ikiwa ni pamoja na kuchimba kisima cha maji katika Shule ya Sekondari, kujenga wodi ya Mama na Mtoto katika kituo cha Afya Mundemu, ujenzi wa barabara kutoka Mundemu kwenda Chilungulu na ujenzi wa nyumba ya mwalimu mambo ambayo hayajatekelezwa na mwekezaji huyo, ila mwekezaji huyo kaanza ujenzi katika eneo la Kijiji bila ridhaa ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Sima ametembelea Wilaya ya Bahi na kuutaka uongozi wa Wilaya hiyo kutenga maeneo maalumu kwa shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu na ile ya Hifadhi ili kunusuru uvunaji holela wa miti ya asili na ile ya kupanda, na kusisitiza ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka katika ulinzi wa rasilimali za misitu na hifadhi ya mazingira.

“Shirikisheni viongozi wa Serikali za Vijiji, tumieni Kamati za Mazingira katika ngazi zote, wakumbusheni majukumu yao mara kwa mara” alisisitiza Mhe. Sima.

Aidha, Mheshimiwa Sima ameagiza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo lindwa ili yaweze kutambulika kwa mujibu wa Sheria na kuutaka uongozi wa Wilaya ya Bahi kuwa na mpango endelevu wa upangaji wa mji wao ili kuwa na ‘Bahi ya Kijani’.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi Bi. Rachel Chuwa amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji hivyo kupelekea miti mingi kukauka katika eneo lao ila jitihada zinaendelea za kupanda miti inayostahimili ukame.

Naibu Waziri yuko kwenye ziara ya kukagua maeneo mbalimbali yanayoathiriwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na uwekezaji holela sambamba na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 katika Wilaya za Chemba, Bahi na Kongwa.