Mifumo ikolojia bora inasaidia kuhimili mabadiliko ya tabianchi – Balozi Sokoine

Mifumo ikolojia yenye afya ndio inaweza kutupatia huduma za uhakika kama chakula, maji safi na salama, kutuepusha na magonjwa, mafuriko, uharibifu wa ardhi na wakati huo huo kutuwezesha kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu kuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine ambaye alikua mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha ya mafunzo kuhusu kuhimili mabadiliko ya tabia Nchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Alisema kuwa Kukosekana kwa huduma hizo kutapelekea kushindwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia (Sustainable Development Goals). Hivyo mradi huu umekuja wakati muafaka wakati pia Serikali ikiendelea kukuza uchumi katika njia endelevu.

“Kama mnavyo fahamu mabadiliko ya tabianchi yameleta athari mbalimbali kwenye mazingira yetu hapa nchini. Kati ya madhara hayo ni kuharibika kwa kanda za Ikolojia Kilimo (Agro Ecolojical Zones) ambazo kwa mujibu wa tafiti kanda hizi ziko saba. Tafiti zinaonyesha kwamba ni rahisi kuhimili (Adaptation) kuliko kukabili (Mitigation)”. Alifafanua Balozi Sokoine.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Bwana Faraja Ngerageza alisema kuwa warsha hiyo itawawezesha washiriki kufahamu zaidi kuhusiana na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia iliyopo vijijini.
Warsha hiyo ya mafunzo ya siku tatu imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia vijini (EBARR). Mradi huu unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Warsha hiyoimehudhuriwa na Washiriki kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, inafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa chuo cha Mipango jijini Dodoma.