SIMUYI KUNUFAIKA NA MRADI MKUBWA WA MAJI

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima ameshuhudia utiaji saini wa Mkataba (Funded Activity Agreement) wa utekelezaji wa mradi wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Sekta ya Maji, Mkoani Simiyu  baina ya Sekretarieti ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) na Benki ya KfW ya Ujerumani. Utiaji saini uliofanyika katika Jiji la Katowice, Poland.

Wakati wa tukio hilo Mhe Sima ameishukuru Bodi na Sekretarieti ya Mfuko huo kwa kuidhinisha fedha za kutekeleza Mradi wa Maji wa Simiyu ni muhimu sana kwa jamii kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu, mifugo na kilimo hususan katika kipindi ambacho athari za mabadiliko ya tabianchi zinazidi kujitokeza.

Mradi huo utatekelezwa katika Mkoa wa Simiyu, na utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 250 ambazo zimetolewa na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi na utekelezaji wake utakamilika katika kipindi cha miaka mitano. Fedha hizo za msaada zimepatikana kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa kuwahi kutolewa na Mfuko huu kimataifa kama msaada katika eneo la kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Aidha, serikali ya Tanzania itachangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa mradi huu.

Vilevile Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuwa mradi huu umekuja wakati muafaka ambapo serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwapatia wananchi maji safi na salama na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Aliwahakikishia kuwa Serikali itasimamia mradi huu katika hatua zake zote za utekelezaji.

Mhe. Mussa Sima yuko nchini Poland akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa 24 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi ulioanza tangu tarehe 2 na utamalizika tarehe 14 Desemba, 2018.