Simbachawene: Mwalimu Nyerere alikuwa mtunzaji mkubwa wa mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. George Simbachawene amesema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa ni mtunzaji mkubwa wa mazingira ingawa enzi za uhai wake suala la mabadiliko ya tabianchi halikuwa changamoto kubwa katika Taifa letu wala ajenda ya ulimwengu kama ilivyo leo.

Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam ambapo alisema mabadiliko ya tabianchi ni ajenda ya dunia na kwa maantiki hiyo Serikali haina budi kuanza kutoa elimu ya kukabiliana na madhara yatokanayo na changamoto hiyo.

Alisema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mtaalamu na mtunzaji wa mazingira ambaye alichochea maendeleo endelevu kwa mfano alizungumzia sheria ya kuhifadhi maeneo yaliyohifadhiwa ikiwa ni pamoja na Hifadhi za Taifa.Aidha, waziri huyo alisema kuwa shughuli za kibinadamu zimekuwa zikisababisha ongezeko la hewa ukaa na kuleta joto kubwa sambamba na mabadiliko ya majira hivyo elimu ikitolewa kwa wananchi italeta tija katika dhana nzima ya utunzaji wa mazingira.

Aliwataka wananchi kutunza mazingira na kusema akuwa kongamano hilo litakalotoa mawazo na mtazamo mpya utakaosaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi huku akibainbisha kuwa uchunguzi wa hivi karibuni unaonesha joto la ardhi katika maeneo mengi ya barani Afrika limeongezeka kwa nyuzi 0.5 hadi 2 katika kipindi cha miaka 50 hadi 100 iliyopita.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuhudhuriwa pia na Balozi wa Norway Bi. Elisabeth Jacobsen lilikwenda sambamba na uzinduzi wa kitabu kinachozungumzia mabadiliko ya tabianchi cha ‘Climate Change and Coastal Resources in Tanzania uliofanyika na Waziri Simbachawene.