Simbachawene azitaka Halmashauri kuweka mpango wa kutoa elimu ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu waRais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa halmashauri zote kuwa na mipango kabambe inayotekelezeka kwa ajili ya kuhakikisha elimu ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi inawafikia wakulima katika maeneo yao.

Pia amezitaka kuwajengea uwezo maafisa ugani kutekeleza jukumu hili muhimu pamoja na kuboresha mawasiliano na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na kuboresha ufikishaji wa taarifa hizi kwa wakulima na maelekezo ya nini wafanye kulingana na hali ya wakati husika.

Simbachawene ametoa wito huo leo Novemba 27, 2019 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa wadau wa kilimo kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na utayari wa nchi katika kukabiliana na changamoto hiyo iliyoandaliwa na Jukwaa Lisilo la Kiserikali la Wadau wa Kilimo (ANSAF).

Alisema mabadiliko ya tabianchi ni tishio duniani huku Tanzania ikiathiriwa na mabadiliko ya misimu na mtawanyiko mbovu wa mvua, ukame na mafuriko ya mara kwa mara, ongezeko la wadudu waharibifu na magonjwa yasiyosikia dawa ya mimea na wanyama, ambavyo vimesababisha wakulima wengi kutopata mavuno ya kutosha na yaliyotarajiwa.

Aliongeza kuwa wanawake na vijana wameonekana kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na ukosefu wa nyenzo za kisasa za kilimo, elimu, kipato kidogo na kushindwa kumiliki ardhi ingawa ndio wenye kufanya kazi kubwa ya uzalishaji.

“Tunaona uharibifu wa vyanzo vya maji husababisha mama zetu na mabinti zetu kutembea umbali mrefu kusaka maji, hii inaweka usalama wao katika mazingira hatarishi na kaya zinapokosa chakula cha kutosha kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, wanawake na watoto ndio waathirika wakuu,” alisema.

Aidha waziri huyo aliwataka wadau wa maendeleo kuhakikisha mbinu zinazotumika katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinakuwa shirikishi na zinazingatia ushiriki thabiti wa wanawake na vijana.

Alitaka pia kuwepo na mikakati kabambe ya kulikwamua kundi hilo na changamoto hii kama vile uchimbaji wa visima katika maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa vyanzo vya maji vimekauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Niwashukuru na kuwapongeza ndugu zetu wa ANSAF kwa kutuleta pamoja ili tujifunze na kushauriana namna bora ya kusaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Nizidi kutoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono juhudi hizi kwa kupeleka miradi ya kilimo stahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima, ili kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha tunafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.