Sima atoa maagizo kwa NEMC

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia upya vibali vya kufanya shughuli ya uwekezaji katika ufukwe wa bahari eneo la Feri mkoani Mtwara.

Sima ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake pamoja na NEMC kwenye mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara kuona namna shughuli za uhifadhi wa mazingira zinavyotekelezwa.

Akitoa maelekezo hayo kuhusu mwekezaji Chandra Shekhar wa kiwanda cha Alpha Krust alitaka NEMC ianze kupitia upya nyaraka ambazo aliombea vibali vya kufanya shughuli hizo katika eneo hilo.

Aidha, alisema baada ya kumsikiliza akidai alipewa vibali kuna haja sasa ya kumhakiki ili aweze kupewa cheti ya mazingira kama atakuwa amefuata sheria za mazingira.

Naibu waziri pia aliagiza uangaliwe upya mpango wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo kuwa yamepangwa yatumikaje ili kama yako sahihi basi apate cheti cha kuendelea na shughuli zake.

“Watu wengu wamekuwa wakiwekeza katika maeneo ya fukwe bila utaratibu na kufanya uharibifu wa mazingira lakini sisi jukumu letu ni kulinda fukwe hizi na ambazo pia ni vyanzo vya sasa kama hatujalinda tutapoteza rasilimali hii ya bahari, hivyo nasitisha kwanza shughuli za mwekezaji huyu hadi pale NEMC watakapofanya review ya vibali vyake,” alisema.

Naibu waziri aliongeza kuwa Sheria ya Mazingira yam waka 2004 57 (2) inampa waziri dhamana ya kuamua ndani ya mita 60 pembezoni mwa bahari nini kifanyike kuendana na mazingira ya eneo hilo lakini si kila shughuli anaweza kuruhusu kufanyika.