Sima atembelea kituo cha Songas Kilwa, atoa maagizo

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima ameagiza kituo cha kupokea gesi asilia cha Songas eneo la Somanga kuwasilisha mpango kazi wa usimamizi wa mazingira unaoonesha madhara na hatua zinazochukuliwa pindi yanapotokea maafa.

Sima ametoa agizo hilo leo wakati wa ziara yake akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Prof. Esnath Chagu na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Samuel Gwamaka kukagua kituo hicho ambacho Novemba 3 mwaka huu kilipata tatizo la kuvujisha bomba la mafuta katika eneo hilo wilayani Kilwa mkoani Mtwara.

Katika ziara hiyo inayohusisha mikoa ya Lindi na Mtwara alisema kuwa ni muhimu wananchi wa vijiji zaidi ya 60 vilivyopitiwa na mradi wa bomba la gesi asilia licha ya kujua faida zake lakini pia wanatakiwa wapate elimu sahihi ya madhara pindi yanapotokea matatizo kama haya.

Aidha, Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi na hasa ya gesi asilia na kutaka mikataba ambayo inaingia na wakandarasi lazima ioneshe wananchi wameshirikishwaje na kuelewa kuhusu madhara yatakajitokeza endapo gesi itavuja.

Alisema kuwa lazima kama nchi tujuie mikataba hii ili kama yakitokea maafa wao wanawajibikaje kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza hususana kwa wananchi wanaopitiwa na miradi hiyo.

“Tumekuja hapa tuone kama mkiradi hii inafuata sheria ya mazingira yam waka 2004 na hapa tunataka tuone kwenye eneo hili yakitokea madhara ni hatua gani zinachukuliwa, tunataka kuona taarifa kamili na tuangalie kwenye eneo letu la mazingira mnachukua hatua gani.

“Hebu turudi kuangalia mkataba huu makubaliano gani tunawekeana sio valvu mpya imetoka maabara imekuja ikawekwa hapa halafu ikajivusha gesi, hapana lazima tuje na majibu sahihi. Natambua wizara husika imefanya kazi yao na sisi tunaoratibu shughuli za mzingira lazima tufanye kazi yetu,” alisema Sima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. chagu alisema ni muhimu kwa watalamu kuhakikisha vifaa vinavyototumika vinakuwa na viwango.

Prof. Chagu alisema kuwa matumizi ya vifaa vyenye viwango yatasaidia katika kuhakikisha matatizo kama haya hayatokei na kuleta madhara kwa wananchi na hata kama yakitokea basi lazima tujue hatua za kuchukua.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai alisema hili ni tukio baya kutokea na kama wasingekuwa makini kuzuia cheche ingekuwa hali ya hatari na kusababisha maafa makubwa.

Ngubiaga alibainisha kuwa katika siku ya tukio hilo wananchi wanaotumia Barabara ya Kilwa hususan wasafiri wa mabasi ya kwenda au kutoka Mtwara na Songea waliathirika kutokana na kutoendelea na safari.

Pia alisema kuwa athari za kiuchumi zilionekana kutokana kuzimwa kwa kituo cha umeme Kilwa kutoka muda wa jioni hadi usiku hivyo wananchi walikosa huduma hiyo na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi.