SIKU YA NNE YA ZIARA YA MAKAMU WA RAIS- SONGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua shamba la miti katika hifadhi ya Misitu Iyondo Mswima lililopo Katengele wilayani Ileje mkoani Songwe ikiwa ni siku ya nne ya ziara yake ya kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani Songwe.

Shamba hilo lililo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ni moja kati ya mashamba mapya yakiwemo Biharamulo (Chato Geita), Buhigwe (Kigoma) na Mpepo (Mbinga, Ruvuma).

Akisoma taarifa ya Shamba hilo kwa Makamu wa Rais, Mkurugenzi wa Mipango –Wakala wa MisituTanzania Bw. Mohamed Kilongo amesema kuwa mpaka shamba la miti la Iyondo Mswima limeweza kutoa ajira kwa wananchi 400 katika msimu wa kupanda miti, pia shamba limetoa ajira zingine 200 wakati huu wa maandalizi ya bustani ya miti, hekta 201 zimepandwa miti kama sehemu ya upanuzi wa mashamba ya miti ya Serikali ambapo bustani yenye jumla ya miche 430,000 kwa ajili ya upandaji miti wa mwaka 2018/2019.

Akizungumza na wananchiwa kijiji cha Katengele ambapo shamba la misitu la Serikali Iyondo Mswima limezinduliwa, Makamu wa Rais amewataka wananchi hao kutunza na kuyalinda mazingira kwa kupanda miti kwa wingi ambapo kila mwaka wananchi watape wa miche 50,000 na Wakala wa Huduma za Misitu wa Serikali.

Makamu wa Rais pia alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Sange ambapo aliwaambia wananchi wa kijiji hicho kuwa Mungu amewapa rasilimali nzuri sana hivyo hawana budi kuyatunza.

Makamu wa Rais amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje kuhakikisha Maafisa Ugani wanashuka kwa wananchi na kutoa ushauri namna yakufanya shughuli za kilimo vizuri.

Makamu wa Rais amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 katika bajeti mwaka huu iliyopita kwa ajili ya kujenga hospitali ya wilaya ya Ileje.

Makamu wa Rais amesema mkoa wa Songwe utapata watumishi 270 katika Sekta ya Afya, na kwenye sekta ya elimu, walimu wengi wameajiriwa mwaka huu ambapo Songwe nayo itapata walimu wapya.

Makamu wa Rais ameandika historia kwakuwa kiongozi wa ngaziz a juu kufika katika vijiji vya Katengele na Sange.