Serikali kuendelea kutoa kipaumbele utekelezaji miradi ya maendeleo

Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kutafuta rasilimali fedha za ndani na nje ili kupanua wigo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

Kauli hii imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Zungu hii leo jijini Dodoma mara baada ya kuwasilisha taarifa ya Ofisi yake kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Ofisi hiyo.

Amesema miradi katika Ofisi yake imechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi; kupunguza uharibifu wa mazingira, kuongeza usalama wa chakula na kuboresha hali ya uchumi kwa jamii; kupunguza uchafuzi wa mazingira na kulinda afya ya jamii.

 

“Umuhimu wa kuhifadhi mazingira unatokana na ukweli kwamba matumizi ya rasilimali za mazingira ndio msingi mkuu wa ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na maendeleo ya Taifa na jitihada za kuondoa umasikini nchini zinaendana na matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira” Zungu alisisitiza.

Amesema changamoto za uharibifu wa Mazingira nchini ni kubwa na kutolea mfano kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa na athari za mabadiliko ya Tabianchi. Ameainisha kuwa ofisi yake imedhamiria kupunguza uharibifu wa mazingira nchini kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala. “Nimeongea na kampuni za usambazaji wa nishati ya gesi hapa nchini ili kupunguza gharama za nishati hili ili kila mwananchi aweze kunufaika nayo na kwa kuanzia kampuni ya Kopa gesi wamekuja na teknolojia ya kuuza gesi kwa reja reja”

Akitoa ufafanuzi juu ya kukithiri kwa magugu maji katika Ziwa Victoria, Waziri Zungu amesema Serikali inaangalia namna bora ya kuvuna magugu maji hayo ili kunusuru viumbe hai na bioanuai inayopatikana katika maeneo hayo.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Murad Sadiq ameishauri Serikali kuweka mkazo katika usimamizi wa Serikali hususan udhibiti wa kelele katika makazi ya watu.

Aidha, Mjumbe wa Kamati hiyo Hawa Mwaifunga ameshauri Serikali kuendelea kutoa elimu ya athari za matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo hapa nchini.

Suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira ni mtambuka, hivyo utekelezaji wake unahusisha sekta zote na jamii kwa ujumla. Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo ni muhimu katika kutatua changamoto za mazingira na ustawi wa jamii ambapo katika mwaka 2019/20 ilipanga kutekeleza jumla ya miradi mitano (5) ya maendeleo.

 

Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa; Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kutekeleza Mkataba wa Montreal Kuhusu Udhibiti wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni; na Mradi wa Kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mkataba wa Stockholm unaohusu Kemikali zinazodumu katika Mazingira kwa Muda Mrefu.

 

Miradi mingine ni pamoja na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kupitia Mifumo ya Ikolojia; na Mradi wa Kusaidia Kujenga Uwezo wa Taasisi na Jamii Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Kwenye Maeneo ya Kaskazini mwa Nchi.