NZEGA YAKABILIWA NA UHARIBIFU MKUBWA WA MAZINGIRA

Changamoto kubwa inayoikabili Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora ni uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na uvunaji holela wa rasilimali za misitu na shughuli za kilimo.

Hayo yamesemwa hii leo na Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bw. Godfrey Ngukuwa wakati akiwasilisha taarifa ya Wilaya yake kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba katika Kijiji cha Ngukumo na Mwambaha, Wilayani Nzega.

“Wilaya yetu imekuwa na ongezeko kubwa la wavamizi kutoka Mikoa jirani wanaojihusisha na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kilimo kisichoendelevu, kwa kiasi kikubwa wanachangia uharibufu wa Mazingira, kwa kuwa hivi sasa Nzega imekuwa soko la Mkaa kwa Shinyanga na Mwanza” alisisitiza Bw. Ngukuwa

Akielezea jitihada zilizofanywa na Ofisi yake Bw. Ngukuwa amesema kuwa doria za mara kwa mara zianaendelea Kijiji hapo kwa kushirikiana na wananchi wenyewe kubaini wavamizi hao.

Nae Waziri mwenye dhamana ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini Mhe. January Makamba amewataka wakazi wa vijiji hivyo kuwa wakali kwa rasilimali zao na kuhakikisha mazingira kwa ujumla wake yanatunzwa kwa sheria kali zaidi.

Pia, ameagiza kufanyika kwa operesheni kali na kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na uharibifu huo. “Ndugu zangu sina budi kuwakumbusha kuwa siku hizi kuna wakimbizi wa Mazingira, watu wanaharibu mazingira katika maeneo yao na kuhamia maeneo mengine, jitihada za maendeleo zote hazitakuwa na maana kama hatutatunza mazingira” Makamba alibainisha.

Waziri Makamba amewaeleza wakazi wa Vijiji vya Ngukumo na Mwambaha kuwa na uhifadhi wenye tija ni ule ambao wananchi wako tayari kushiriki kwa nguvu zote. Katika kuunga mkono shughuli za maendeleo, Waziri Makamba amechangia kiasi cha Shilingi Milioni Moja kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati na matundu ya Choo katika Shule ya Msingi Mwambaha.

Waziri Makmaba amehitimisha ziara yake Mkoani Tabora na amewasili Mkoani Geita ambapo atatembelea Kisiwa cha Magafu.