NAIBU WAZIRI SIMA AAGIZA GEREZA LA ISANGA KUTUMIA NISHATI MBADALA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima hii leo amefanya ziara ya kikazi katika Gereza Kuu la Isanga lililopo Jijini Dodoma na kuutaka uongozi wa Gereza hilo kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa kupanda miti zaidi na kuacha  matumizi  yasiyoendelevu ya mkaa na kuni kama nishati ya kupikia.

Akizungumza na Uongozi wa Gereza hilo Mhe. Sima amewataka kutumia majiko banifu ili kupunguza kasi ya ukataji miti kwa matumizi ya kupikia. “Natoa wito kwenu kuanza kutumia teknolojia mbadala ya kuni na mkaa kama nishati ya kupikia na kuwaagiza kuona namna bora ya kutumia gesi ili kunusuru misitu yetu”

Pia, Waziri Sima ameagiza uongozi wa gereza hilo kutenga eneo maalumu kwa ajili ya kuotesha miti inayostahimili ukame kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na shamba darasa kwa watu kujifunza kilimo hicho cha miti na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Akitoa taarifa ya Gereza hilo Naibu Kamishna wa Magereza Julius Mayenga Sang’udi amesema kuwa kwa siku gereza hilo hutumia wastani wa kuni mita za ujazo 8-10 kwa matumizi ya kupikia, kuni ambazo hutolewa katika kambi ya Mayamaya, Taasisi za Serikali na ujenzi binafsi.

Kufuatia maelekezo ya Naibu Waziri, Kamishna Sang’udi amesema kuwa mpango uliopo sasa ni kugeuza changamoto kuwa fursa ikiwa ni pamoja na kuhuisha wazo la kujenga mfumo wa matumizi ya gesi na ‘biogas’ kama nishati ya kupikia.

Katika hatua nyingine Waziri Sima ametembelea Ranchi ya Kongwa na kumuagiza Meneja wa Ranchi hiyo Bw. Euzebius Mutayabirwa kuandaa mpango maalumu wa uoteshaji wa miti katika eneo lao haraka iwezekanavyo, na kuwaomba Wakala wa Misitu Tanzania kupeleka miti katika eneo hilo yenye kuhimili ukame na rafiki kwa mazingira.

“haiwezekani eneo kama hili lenye ufugaji mkubwa, eneo lenye ngo’mbe zaidi ya 9000 lakini hamuwezi kupanda miti wakati mnataka kutunza vyanzo vya maji, eleweni kuwa ufugaji ni sambamba na kutunza mazingira. Inawezakanaje kuwa na ufugaji  kama huu halafu hakuna mpango wowote wa upandaji wa miti?” Waziri Sima alihoji.

Sambamba na hilo Mhe. Sima amemwagiza Meneja wa Ranchi hiyo Bw. Mutayabirwa kuwa mfano kwa kuwa na shamba darasa la matumizi ya ‘Biogas’

Nae Meneja wa Ranchi hiyo Bw. Mutayabirwa amesema kuwa utekelezaji wa maagizo hayo unaanza mara moja ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti kwa ajili ya vivuli vya mifugo na kuhifadhi vyanzo vya maji na kuwashirikisha wataalamu wa Carmatec kwa ajili ya kukamilisha andiko la mradi wa kuzalisha biogas.

Naibu Waziri Sima amekamilisha ziara yake ya siku tatu kwa kutembelea Wilaya za Chemba, Bahi na Kongwa zote za Jijini Dodoma.