MIRADI YA MAENDELEO KUTUMIA FEDHA ZA NDANI – MHE. MAKAMU WA RAIS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema vituo vya afya 350 vitakuwa vimekamilika nchi nzima ndani ya miaka mitano ya Uongozi wa Awamu ya tano. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati alipotembelea kituo cha afya cha Sokoine wilayani ya Singida mkoa wa Singida ikiwa muendelezo wa ziara yake ya kikazi ambapo amekuwa akikagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo.

“Kulikuwa na hospitali 65 za wilaya lakini tulivyoingia madarakani zimejengwa hospitali 67 na lengo kuu ni kuwapa wananchi huduma bora ya afya” alisema Makamu wa Rais.

Aidha Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitokubalina na misaada ya masharti na imejidhatiti kufanya miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha zake za ndani. 

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Rais alizindua barabara ya Karume ambayo inajumuisha mradi wa mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 6.1 ambazo nibarabara ya Karume yenyewe , Boma Kinyeto, Double Road Junction (Semali Singida-Dodoma ). Sambamba na hayo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alitembelea kituo cha afya Migori ambapo alijionea maendeleo ya ujenzi ambao unatazamiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi machi, pia alitembelea shule ya sekondari ya Mwanamema Shein ambapo alizungumza na wanafunzi na kujionea maendeleo ya ujenzi wa bweni la wanafunzi pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa maji ameahidi kutoa tanki la maji la lita 10,000 kwa ajili ya kituo cha afya cha Karume ikiwa kama jitihada za kumuunga mkono Makamu wa Rais ambaye amejitoa kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa salama.