Mhe Samia:Wakuu wa Nchi AU wakubaliana uanzishaji Eneo Huru la Biashara

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika (AU) wamekubaliana kupitisha uanzishaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika.

Mhe. Samia amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 12 wa Dharura wa AU uliofanyika mjini Niamey nchini Niger akimwakilisha Mhe. Rais Dkt John Magufuli.

Alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kukubaliana na kupitisha yale yote yaliyokubaliwa na kupitishwa katika vikao mbalimbali vya wataalamu na mawaziri katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya Eneo Huru la Biashara barani humo.

“Tumemaliza awamu ya kwanza na mkutano huu umepitisha vipengele vyote vya awamu ya kwanza lakini pia tumeombwa wataalamu wakakae waangalie yale yaliyobakia ambayo ni ya awamu ya pili nayo tukubaliane tena katika mkutano mwingine utakaofanyika Januari mwakani,” alisema.

Makamu wa Rais alisema kuwa AU imepitisha kuwepo kwa eneo hilo la biashara pamoja mifumo mitano itakayosaidia kufanya uendeshaji wa biashara huru ndani ya Afrika.

Mifumo hiyo alitaja kuwa ni pamoja na kuondoa vikwazo ambavyo si za kikodi lakini na pia wamepitisha mfumo utakaoweza kufanya tathmini, kuripoti na kufuatilia utekelezaji wa mfumo huo.

“Pia tumetakiwa katika jumuia zetu za kikanda sasa kwa upande wetu kupitia SADC (Jumuiya ya Kibiashara ya Nchi za Kusini mwa Afrika) na Afrika Mashariki (EAC) twende tukajipange tuiangalie mifumo tuliyopitisha tuangalie zina changamoto gani na vipi tunaweza kusaidiwa,” alisema.

Mhe. Samia katika mkutano huo aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Damas Ndumbaro na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Mohamed Ramia