Mhe. Kangi Lugola ametoa muda wa miezi sita kwa kiwanda cha HUACHENG

Naibu Waziri  Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Kangi Lugola ametoa muda wa miezi sita kwa kiwanda cha HUACHENG kinachojihusisha na uchinjaji na usafirishaji wa nyama ya Punda Mkoni Dodoma kuondoa mabaki ya miundo mbinu ya vyuma na mbao ambavyo awali vilikua vikitumika katika uchinjaji wa ngo’mbe.

Mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika kiwanda hicho iliyolenga kufuatilia maagizo ya Serikali yaliyotolewa hapo awali, Waziri Lugola ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kutafuta wawekezaji ambao wanaweza kutumia miundo mbinu hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. “Mvua itakaponyesha mahali hapa patakuwa na uchafuzi wa hewa, na kwetu sisi wana mazingira magofu kama haya ni uchafuzi wa mazingira, hivyo ndani ya miezi sita kama hamjapata ufumbuzi, ondoweni mabaki haya”. Lugola alisisitiza.

Aidha, Kiwanda hicho kimetakiwa kufuata takwa la kisheria la kufanya Ukaguzi wa Mazingira kwakuwa awali kiwanda hicho kimekua kikifanya shughuli zake bila kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira. Waziri Lugola ameupa uongozi wa Kiwanda hicho muda wa miezi miwili kukamilisha takwa hilo kama lilivyoainishwa katika Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.

Katika ukaguzi huo Waziri Lugola amegundua pia kiwanda hicho hakina Mpango Endelevu kama Sheria inavyoelekeza, hivyo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC limeagizwa kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo ndani ya miezi miwili.

Msemaji wa Kiwanda hicho Bw.Michael Gao amesema kuwa maagizo hayo yatatekelezwa kikamilifu na kwa muda uliotolewa.

Kiwanda hicho huchinja punda ishiriki kila siku na wanasafirishwa kupelekwa katika Nchi za China na Vietnam.