MASWALI YANAYOULIZWA MARA KWA MARA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

 KATAZO LA SERIKALI KUHUSU UZALISHAJI, UINGIZAJI, USAFIRISHAJI NJE YA NCHI, USAMBAZAJI, UUZAJI NA MATUMIZI YA MIFUKO YA PLASTIKI

(FREQUENTLY ASKED QUESTIONS)

 • KATAZO LINAHUSU NINI?

Katazo hili linahusu kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ya aina zote.

 • KATAZO HILI LINAANZA LINI

Katazo hili linaanza tarehe 1 Juni,2019.

 KWA NINI SERIKALI IMEAMUA KUPIGA MARUFUKU MIFUKO YA PLASTIKI?

Serikali imeamuakupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ili kuepusha athari za kiafya na mazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo. Athari za mifuko ya plastiki ni pamoja na kutooza katika mazingira kwani inakadiriwa kudumu hadi zaidi ya miaka 500 na hivyo kuleta athari za muda mrefu; uchafuzi wa mazingira hasa kwa mifuko hii kuzagaa ovyo katika mazingira; kuziba miundombinu ya majitaka na mifereji ya mvua na kusababisha mafuriko; kuharibu mfumo wa ikolojia na bioanuai, vifo vya mifugo na wanyama wengine hususan mifugo na viumbe wa baharini wanapokula na kumeza mifuko hii.

 • BIDHAA GANI ZA PLASTIKI AMBAZO HAZIHUSIKI NA KATAZO HILI?

Bidhaa ambazo hazitaathiriwa na katazo hili ni pamoja na vifungashio vya bidhaa kama vile vifungashio vya madawa, vifungashio vya vyakula kama vile: maziwa, korosho, n.k bidhaa za viwandani, kilimo na ujenzi. Hata hivyo, vifungashio ni lazima vikidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

 • KATIKA KIPINDI CHA MPITO, SHEHENA YA MIFUKO YA PLASTIKI ZITASALIMISHWA VIPI?

Utaratibu maalumu unafanywa ambapo kila Wilaya itatenga eneo maalum la kukusanyia mifuko ya plastiki na umma utatangaziwa maeneo hayo.

 • ADHABU KWA ATAKAYEKIUKA KATAZOHILI NI NINI?

Adhabu mbalimbali ikiwemo faini au kifungo gerezani zitahusika kwa atakayekiuka katazo hili kulingana na Kanuni za “Marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki za Mwaka 2019” zilizoandaliwa chini ya Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.

 • MBADALA WA MIFUKO YA PLASTIKI NI NINI?

Mbadala wa mifuko ya plastiki ni mifuko kama vile karatasi, nguo, vikapu, gunia n.k. Mifuko hii ni ile ambayo ni rafiki kwa mazingira kwani inapoisha muda wake huoza katika mazingira. Mifuko hii haina madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

 • UZALISHAJI WA MIFUKO MBADALA UNATOSHELEZA MAHITAJI?

Uwezo na utayari wa uzalishaji wa mifuko mbadala  ni wa kuridhisha. Kwa sasa vipo viwanda vya karatasi 25 hapa nchini. Aidha, tayari kuna viwanda ambavyo vinazalisha mifuko mbadala ya karatasi, nguo na mingineyo ambavyo vinatarajia kuongeza kiwango cha uzalishaji katika muda mfupi kuanzia sasa. Vilevile kuna kundi la pili ni la wawekezaji na wamiliki wa viwanda ambao walikuwa wanasubiri tamko la Serikali ili waweze kuwekeza mara moja katika uzalishaji wa mifuko mbadala. Kundi la tatu ni lile la viwanda ambavyo vinazalisha kwa ajili ya soko la nje zaidi ikiwemo kiwanda cha Mufindi Paper Mills (MPM) – Iringa ambacho huzalisha malighafi za karatasi katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar na Zambia. Ambao tayari wameihakikishia Serikali kuzalisha kwa wingi malighafi za kutosheleza watengenezaji wa ndani wa mifuko ya karatasi.

 • TAARIFA ZA UWEKEZAJI KATIKA UZALISHAJI WA MIFUKO MBADALA ZINAPATIKANA WAPI?

Ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima kwa wenye nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki, wawasiliane na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC);  Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (NEMC);  Shirika la Viwango Tanzania  (TBS); Shirika la Maendeleo la Viwanda Vidogo (SIDO) na Taasisi za Fedha.

 • SERIKALI IMEJIPANGAJE ILI KUHAKIKISHA KATAZO HILI LINATEKELEZWA IPASAVYO?

Mpaka sasa Serikali imefanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha katazo hilo linatekelezwa kwa ufasaha. Pamoja na masuala mengine mpaka sasa yafuatayo yamefanyika:

 • Serikali imeandaa Kanuni za “Marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki za Mwaka 2019” zilizoandaliwa chini ya Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 ili kulipa katazo hili mamlaka ya kisheria;
 • Kuunda Kikosi kazi cha Serikali kinachojumuisha Taasisi zote (National Task Force) chenye majukumu tofauti  kinachoratibiwa na OMR na NEMC;
 • Taasisi zinazounda Kikosi Kazi hicho ni pamoja na: TAMISEMI; Ofisi ya Makamu wa Rais; Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji); Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka; Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii,Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi – Idara ya Uhamiaji; Idara ya Usalama wa Taifa – (TISS); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali; Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira; Mamlaka ya Bandari Tanzania; Shirika la Viwango Tanzania; Mamlaka ya Chakula na Dawa; Mamlaka ya Viwanja vya Ndege; Mamlaka ya Mapato Tanzania; Jeshi la Polisi Tanzania; na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.
 • Pamoja na masuala mengine, majukumu ya kikosi kazi ni pamoja na: kutoa elimu kwa umma; kuratibu ufuatiliaji na uzingatiaji wa Sheria na Kanuni husika; kudhibiti wazalishaji, wasambazaji,watumiaji, wauzaji wa mifuko ya plastiki; Kuandaa viwango vya ubora wa mifuko inayoruhusiwa kisheria; Kudhibiti uingizaji nchini na usafirishaji nje ya nchi wa mifuko ya plastiki; na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa mifuko mbadala.
 • Kuendesha kikao cha wadau mbalimbali ili kujadili fursa za uwekezaji wa uzalishaji wa mbadala wa mifuko ya plastiki;
 • Kuandaa Mpango Kazi wa utekelezaji wa katazo husika.
 • Elimu kwa Umma ili kuhakikisha wananchi wote wanapata taarifa sahihi na kwa wakati. Pia kuhimiza wawekezaji kuongeza kasi katika uzalishaji wa mifuko mbadala.

WITO

Ili kwenda sambamba na Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Kujenga Uchumi wa Viwanda na wakati huo huo kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali inatoa wito kwa Wadau wote ikiwemo wawekezaji katika viwanda kuzingatia umuhimu wa uchumi wa mbadala wa mifuko ya plastiki kwani  utawezesha ajira nyingi zaidi na kukuza kipato kwa wananchi wa kawaida hasa kina mama katika kutengeneza mifuko mbadala ambako kunahitaji teknolojia rahisi na nguvu kazi.