MAKATIBU WAKUU WA SADC KUJADILI MIKAKATI YA KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Makatibu Wakuu kutoka  Sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za SADC wameanza vikao vya kujadili na kuweka agenda za mkutano wa Mawaziri wa sekta husika kutoka umoja huo ambapo wanatarajia kujadili mpango mkakati wa pamoja wa kukabiliana na ujangili ili kutomokeza ujangili katika nchi mwanachama na kuweka jitihada za pamoja za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolfu Mkenda akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa makatibu wakuu kutoka nchi mwanachama  amesema kuwa mkutano huo utajadili mambo mbalimbali ikiwemo vita dhidi ya ujangili ambayo inapaswa kuungwa mkono kwa nchi zote mwanachama badala kuachwa kwa nchi moja.

Mkenda amesema kuwa nchi moja ni vigumu kupambana na ujangili hivyo tunahitaji kuunganisha nguvu kwa nchi zote ili ziweze kufanikisha juhudi za kupambana na ujangili.

“Tunahitaji kuwa na mpango mkakati wa kukuza utalii katika nchi za SADC  hii ni moja kati ya ajenda muhimu zitakazojadiliwa” Alisema Profesa Mkenda

Mkurugenzi wa idara ya Chakula ,kilimo na Maliasili kutoka Sektretarieti ya SADC ,Domingos Zephania Gove amesema kuwa wanahitaji kutembea pamoja kama nchi za SADC katika kuweka mikakati katika masuala ya kimazingira,Utalii na Wanyamapori .

Gove amesema kuwa wanahitaji kuthibitisha program za pamoja za kukuza utalii na kusimamia maliasili katika ukanda husika.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amesema, Mkutano wa  Mawaziri wanaosimamia sekta za  Mazingira, Maliasili na Utalii utajadili masuala muhimu ikiwa ni pamoja na:- Mwenendo wa uridhiaji wa Itifaki ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu Protocol on Environmental Management for Sustainable Development; Mabadiliko ya Tabianchi; Kuundwa kwa Mkakati wa SADC wa Uchumi wa Bahari (SADC Strategy on Blue Economy); Mpangokazi wa SADC wa Kudhibiti Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (SADC Action Plan to Combat Desertification); Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa inayohusu Hifadhi ya Mazingira ambayo SADC ni mwanachana; Mikakati ya utafutaji wa fedha za kutekeleza masuala hifadhi ya mazingira na Hali na mwenendo wa utekelezaji wa sekta ya misitu, wanyamapori na utalii.

“Sote tunakubaliana kuwa bila Mazingira hakuna Maendeleo endelevu, tunaweka malengo ya kulinda rasilimali zetu kwa pamoja ambazo zinavuka mipaka mfano mito, misitu, maziwa” Malongo alisisitiza.