MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA WILAYA YA BUHIGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wakazi wa Kigoma kujihadhari na utapeli unaoendelea ambapo vimetokea vikundi vya watu vikiandikisha majina kwa ajili ya kupatiwa milioni 50 kila kijiji.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi wa kijiji cha Munzenze wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

“Nimepata taarifa kwamba kuna wajanja wanakuja wanapitia Vijitaasisi vilivyoko huku ndani wanakuja kuchangisha pesa wanawaambia mtoe pesa na wale watakaotoa ndio watakaokuwa wa kwanza kupewa milioni 50 za kila kijiji zinazotoka Serikalini, nataka kuwaambia huo ni uongo hao ni matapeli wanakuja kuchukua pesa yenu, wengine walidiriki kusema tumetumwa na Makamu wa Rais, sijawatuma sijawatuma kwa hiyo mtu yeyote anayekuja kukusanya pesa kwa ajili hiyo kamateni mwitieni polisi” alisema Makamu wa Rais,

Aidha alisema Serikali kwa sasa inashughulikia Hospitali, Vituo vya Afya, Maji, Umeme lakini pia anatambua Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeamrisha wafanye na watafanya ila kwa sasa bado.

Katika siku ya nne ya ziara yake mkoani Kigoma, Makamu wa Rais alipata nafasi ya kutembelea shamba la miti Buhigwe na kupanda mti wa kumbukumbu ambapo pia alipata nafasi ya kuwasalimu wananchi.

Makamu wa Rais aliwahimiza wananchi wa Buhigwe umuhimu wa Lishe Bora kwa watoto, kupima afya, umuhimu wa kujiandikisha bima ya afya, faida za kupanda miti na kutunza mazingira na kuchagua viongozi wachapa kazi.

Katika ziara yake leo wilayani Buhigwe Makamu wa Rais aliongozana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Technolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe Ndugu Albert Obama, Mbunge wa Viti Maalum Vijana anayewakilisha mkoa wa Kigoma Bi. Zainab Katimba, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya mkoa na Chama.