MAKAMU WA RAIS AENDELEA NA ZIARA YAKE BAGAMOYO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya awamu ya tano imeendelea kutekeleza ahadi ya kusambaza maji mjini na vijijini ambapo mpaka ifikapo mwaka 2020 inategemea maji yatakuwa yamefika vijijini kwa asilimia 85% na mjini asilimia 90%.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa tanki kubwa la mradi wa maji Bagamoyo lenye uwezo wa kubeba lita milioni 6 ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku sita mkoani Pwani.

Makamu wa Rais ameipongeza Dawasa kwa kazi nzuri na amewataka wananchi kupitia kamati mbali mbali za maji kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji, miundo mbinu pamoja na mazingira yake.

“Wote tujitahidi kutunza vyanzo vya maji”alisema Makamu wa Rais

Tenki hilo la Bagamoyo linatarajiwa kuhudumia wakazi wote wa mji wa Bagamoyo na vitongoji vyote vinavyozunguka mji huo.

Makamu wa Rais pia alipata nafasi ya kutembelea mradi wa uzalishaji na usambazaji vifaranga wa kampuni ya AKM Glitters na kuzungumza na wananchi waliojitokeza kwenye viwanja vya shule ya msingi Majengo.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais aliongozana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu na vIongozi wengine wa Chama na Serikali.