MAFANIKIO YA OFISI YA MAKAMU KWA KIPINDI CHA MIAKA MITATU

Naweza kuanza kwa kusema kuwa ama kweli kila zama na mambo yake, nimetumia msemo huu ili kujenga hoja ya namna ambavyo uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisaidiwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wanavyoshirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na jemedari Dkt. Ally Mohamed Shein walivyofanikiwa kuimarisha Muungano wetu.

Pamoja na kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu katika kutekeleza majukumu ya kuwaletea wananchi wake maendeleo makala hii inaangazia zaidi utekelezaji wa ahadi za Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia masuala ya Muungano na Mazingira na namna ambavyo imetekeleza kwa vitendo ahadi hizo.

Makala hii ina sehemu kuu mbili ambapo moja inahusu masuala ya Muungano na sehemu nyingine inahusu Uhifadhi na Usimamizi wa mazingira, hata hivyo katika kukamilisha makala hii itakuwa na sehemu ndogo ya hitimisho itakayohusu masuala mtambuka.

Muungano Wazidi Kuimarika

Itakumbukwa kuwa Tanzania ni nchi ambayo imetokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mnamo mwaka 1964 baada ya waasisi wetu kuona ipo haja ya kuwepo kwa Muungano huu kwa sababu mahususi ambazo mpaka leo umeendelea kuenziwa na kulindwa na kuimarishwa.

Kipaumbele cha kwanza  kimeendelea kuwa ni; kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa yenye umoja, amani na usalama, na Muungano wetu unaendelea kudumu na kuimarika.

Katika jambo lolote lile jema hapakosi kuwa na changamoto za hapa na pale, hivyo kumekuwapo na changamoto kadhaa katika muungano wetu ambazo zimekuwa zikishughulikiwa na viongozi wetu wa awamu zote zilizopita.

Kutokana na uwepo wa changamoto hizo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa na dhamira ya dhati kuhahikishi inaendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kuhakikisha ushirikiano huo unazidi kuimarika.

Kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, chini ya uongozi Mahiri wa Mama Samia Suluhu Hassan,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imekuwa ikiratibu na kuendesha vikao vya kisekta vya ushirikiano kwa Wizara, Idara na Taasisi zisizo za Muungano kwa lengo la kubaini na kutatua changamoto, kuleta ufanisi na uwiano wa maendeleo kwa pande mbili za Muungano. Vikao hivyo vimekuwa vikijadili masuala ya kisekta kwa kubadilishana ujuzi, utaalamu na uzoefu kupitia mafunzo, masuala ya sera na ushiriki katika masuala ya kimataifa.

Kufuatia kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika mazingira, Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ imeendelea kuzitafutia ufumbuzi hoja zilizobakia chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo tarehe 27 Novemba 2017, Ofisi ilizikutanisha sekta za Fedha, Uchukuzi na Biashara ili kuendelea kutafuta ufumbuzi wa hoja za sekta hizo.

Katika sekta za fedha hoja zilizojadiliwa zilikuwa ni pamoja na; Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki; Taarifa ya Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha; na Mgawanyo wa mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.

Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ vimekuwa ni nyenzo muhimu ya kusaidia kupunguza changamoto za Muungano.  Aidha, changamoto zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi ambazo ni: Mgawanyo wa mapato ya kodi na misaada; Usajili wa vyombo vya moto; Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu; na Taarifa ya mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha.

Aidha Serikali inaendelea kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha uchumi katika pande zote mbili za Muungano hususan katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya pande zote.

Serikali inaendelea kutekeleza miradi na program za pamoja zinazotekelezwa katika pande zote mbili za Muungano. Miradi hiyo ni pamoja na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tanzania Social Action Fund- TASAF III), Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) na Mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kanda ya Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (South West Indian Ocean Fisheries Governance and Shared Growth-SWIOFISH)

Katika kuhakikisha tunaendelea kuulinda Muungano wetu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imekuwa ikiendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu na faida zinazotokana na Muungano kupitia vyombo vya habari ikiwemo redio, televisheni na magazeti. Makongamano manne yaliyohusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo yalifanyika kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya Muungano kwa vijana ambao ni taifa la leo/kesho, ambao wengi wao wamezaliwa baada ya Muungano.

Harakati hizo za kuulinda na kuutetea Muungano zinafanywa kwa kuzishirikisha Asasi zisizo za Serikali kwa kuimarisha utoaji wa elimu ya uraia mashuleni, vyuoni na vyuo vikuu pamoja na makundi mengine.

Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira Waimarika;

Sekta  zote  za  uzalishaji  mali zinategemea mazingira. Hivyo, rasilimali zitokanazo na mazingira zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi. Hata hivyo, shughuli zisizo endelevu za uzalishaji mali zimechangia kwa kiasi kikubwa katika Uharibifu wa ardhi; Ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini; Uchafuzi wa mazingira; Upotevu wa bioanuai na makazi; Uharibifu wa mifumo ikolojia ya majini; Uharibifu wa misitu; na Mabadiliko ya tabianchi;

Kupitia utekelezaji wa matakwa ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004 Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikekeleza wajibu wa kuhakikisha inatunza na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo ya wananchi.

Moja ya njia ya kutunza na kuyalinda mazingira yetu ni kulinda uoto wa asili ambao ndiyo kichocheo cha kulinda mabadiliko ya tabia nchi, kutokana na umuhimu huo Serikali ya Awamu ya Tano imeelekeza mikoa yote kupanda miti takribani 1.5 milioni kila mwaka ili kuendeleza ukijani wa asili nchini.

Katika kutia chachu dhima hiyo Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya upandaji miti mkoani Dodoma mnamo tarehe 21 Desemba, 2017 ikilenga kubadilisha mji wa Dodoma kuwa wa kijani, na kufuatiwa na zoezi kama hilo lilofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo takriban miti 30,000 ilipandwa mwezi Januari mwaka huu.

Aidha Serikali inaendelea kuweka mkazo kwa Halmashauri zote nchini kuwa na sheriaa ndogo na kanuni zake kwa lengo la kurahishisha usimamizi wa utunzaji wa mazingira kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, ikiwa ni pamoja na  uanzishwaji wa Kamati za Mazingira katika ngazi zote za Serikali, kuanzia ngazi ya kijiji, mtaa, Kitongoji hadi kata.

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utunzaji wa mazingira katika Serikali ya Awamu ya Tano kusimamia uhifadhi wa mazingira ni pamoja na; Wananchi walishirikishwa kupanda na kuhifadhi mikoko kwenye maeneo ya miradi ya kuhifadhi fukwe ambapo jumla ya hekta 1,015.2 za mikoko zimepandwa katika maeneo ya Pwani na kugharimu kiasi cha shilingi 657,346,453.62.

Ujenzi wa ukuta  katika ufukwe  wa Bahari ya Hindi umekamilika ambapo katika eneo la Barabara ya Obama  mita 920 zimejengwa na chuo cha Mwalimu Nyerere mita 500 zimejengwa ujenzi uliogharimu jumla ya shilingi 7,609,364,080

Mafanikio mengine ni ujenzi wa ukuta katika  ufukwe wa mto  Pangani  ambapo umefikia mita 641 kati ya 950 na Kisiwa Panza ujenzi wa mita 40 umekamilika na kugharimu shilingi ni 4,070,853,364,

Ujenzi wa miradi hiyo ni utekelezaji miradi miwili ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi  ambayo ni Mradi wa Kujenga Uwezo wa Jamii za Pwani Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi; na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Jiji la Dar es Salaam. Miradi hii iko chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi na Itifaki ya Kyoto.

Katika hatua nyingine Serikali imeandaa Mkakati wa Kutunza na Kuhifadhi Rasilimali za Bahari, Pwani na Fukwe (The National Integrated Coastal Environmental Management Strategy 2003 – NICEMS)  ambapo mafunzo kwa Halmashauri 16 yamefanyika na maandalizi ya Mpango Kazi, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa miradi, kufanya tafiti kuhusu mmomonyoko wa ardhi na tathmini ya mazalia ya viumbe ndwele/adimu.

Kutokana na umuhimu wa utunzaji wa mazingira Serikali imeandaa utaratibu wa kupunguza bei ya gesi na majiko yake na kuhamasisha jamii kutumia umeme na nishati mbadala ili kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati hizo kutoka asilimia 36 mwaka 2015 hadi asilimia 50 mwaka 2020 ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa lengo la kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira

Katika kuonyesha njia na kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati mbadala Serikali imesambaza majiko banifu 3,000 kwa kaya maskini katika wilaya ya Kinondoni, Temeke na Ilala sambamba na utoaji elimu kuhusu matumizi ya majiko hayo. Gharama 139,351,295. Taasisi kubwa za Serikali pia zimehamasishwa kutupunguza matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kuweka miundombinu rafiki ya matumizi ya gesi na tungamotaka.

Ofisi ya Makamu wa Rais, kupitia Baraza la Usimamizi wa Mazingira NEMC limetoa cheti cha Tathmini ya Athari ya Mazingira kwa ajili ya mradi wa Ufuaji wa Umume katika Bonde la Mto Rufiji unaotarajiwa kuzalisha umeme mega wati 2100 zitakazopelekea kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa.

Hivyo,  kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingara  Na. 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 81, mradi huu umefanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira ili kubaini matokea hasi na chanya na kuweka mipango ya kudhibiti madhara na kuboresha utekelelezaji wake. Aidha Serikali imeanza mchakato wa kufanya Tathmini ya Mazingira Kimkakati (TMK) katika bonde zima la mto Rufiji kuanzia ukanda wa juu mpaka ukanda wa chini.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano madarakani, Baraza limeendelea kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa shughuli za viwanda ili zisiharibu mazingira. Serikali imeandaa   Mwongozo wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati (National Guidelines for Strategic Environmental Assessment 2017) ambao unawezesha mipango ya ujenzi wa uchumi na viwanda kufanyiwa tathmini ya mazingira kimkakati ili kuhakikisha kuwa uchumi wa viwanda unakuwa endelevu.

Jumla ya kaguzi za viwanda 1869, migodi 128, na maeneo mengine 937 umefanyika ikiwa ni muendelezo wa usimamizi wa athari za mazingira zitokanazo na shughuli za viwanda na migodi.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira linaendelea kusimamia na kutekeleza shughuli za uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sura 191 na Kanuni zake kwa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi 627 katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Pwani, Morogoro, Kigoma, Tabora, Dar es Salaam, Tanga, Geita, Mwanza, Dodoma, Songwe, Iringa, Lindi, Kagera, Mbeya, Ruvuma, Singida, Mara, Shinyanga, Simiyu na Mtwara.

Aidha miradi 179 iliyokiuka Sheria ilichukuliwa hatua stahiki. Hatua hizo ni pamoja na kutoa maelekezo, maonyo, amri za katazo, amri za urejeshaji wa mazingira na baadhi walifikishwa mahakamani. Baraza litaendelea kufanya ukaguzi na ufuatialiji wa miradi ya uwekezaji na kuchukua hatua stahiki kwa wataokiuka Sheria hiyo.

Pamoja na mafanikio hayo Ofisi ya Makamu imefaniwa Kuanzisha mfuko wa mazingira na kuteua Wakaguzi wa Mazingira ambapo jumla ya Wakaguzi wa Mazingira 533 wameteuliwa  kwamujibu wa  Sheria ya mazingira na kati ya hawa 435 ni kutoka katika Halmashauri za Miji na Majiji kwa lengo la  kuboresha ukaguzi wa mazingira na ufuatiliaji na utekelezaji wa Sheria.  Aidha, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeanzisha utaratibu wa kutoa kibali cha muda cha mazingira ili kuharakisha utoaji wa kibali cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kwa miradi mbalimbali.  Kwa utaratibu huu miradi ya viwanda pamoja na ile itakayosajiliwa Tanzania Investment Centre (TIC) itapewa kibali cha muda wakati mchakato wa TAM unaendelea, ambapo jumla ya Vyetii 2,099 vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) katika kipindi cha miaka miwili (2015-2018).

Kufuatia kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyotoa tarehe 16/02/2017 huko Mererani, Mkoani Manyara kuhusu kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi 2017, Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya kuratibu Operesheni Maalum ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali na kuchukua hatua stahiki. Kikosi Kazi maalum katika Operesheni hii  kilikagua na kuzuia (seize) pombe kali zilizofungashwa katika viroba (sachets) kwenye viwanda na kuorodhesha idadi ya pombe za viroba zilizopo, vifungashio (packaging materials), Kukagua na kuzuia pombe kali zilizofungashwa katika viroba (sachets) kwenye maghala (warehouse /store), na maduka ya jumla (whole sale) na kuorodhesha idadi ya pombe kali zilizofungashwa katika viroba na vifungashio (packaging materials) tupu vilivyopo; Kukagua uhalali wa vibali na nyaraka za uzalishaji /uendeshaji wa kiwanda /msambazaji husika (mfano vibali na vyeti vya TFDA na TBS, EIA, stempu za kodi za TRA, leseni za biashara, leseni za vileo).

Aidha, katika kutekeleza operesheni hii maalum, Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Kanuni ya Kukataza Uzalishaji, Uingizaji na Matumizi ya Vifungashio vya Plastiki kufungia Pombe Kali, iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali Namba 76 ya mwaka 2017. Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura, 191 pamoja na Kanuni ya Kukataza Uzalishaji, Uingizaji na Matumizi ya Vifungashio vya Plastiki kufungia Pombe Kali ya mwaka 2017 zilitumiwa katika kutekeleza Operesheni hii. Operesheni hii ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa maana mpaka sasa viroba ambavyo vilikuwa vinathari kwa mazingira na jamii kwa ujumla havipo tena.

 

Ofisi ya Makamu wa Rais tukiwa waratibu na wasimamizi wa Mazingira Nchini, tunatekeleza Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambapo miradi kadhaa imeandaliwa, ikiwa ni pamoja na Mradi wa Usimamizi wa Matumizi Endelevu ya Ardhi ya Bonde la Ziwa Nyasa. Mradi unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) kupitia Umoja wa Kimataifa wa hifadhi ya Mazingira (UNEP). Mradi huu utagharimu kiasi cha dola za kimarekani 1,298,980  na unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na utatekelezwa na Halmashauri za Wilaya tano (5) zilizoko kwenye Bonde la Ziwa Nyasa, pamoja na taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali. Wilaya zinazoshiriki kutekeleza mradi huu ni pamoja na Ludewa, Kyela, Makete, Nyasa na Mbinga. Aidha, wadau wengine watakaoshiriki katika kutekeleza mradi huu ni pamoja na Chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA); Tume ya Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na maendeleo ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na NGOs zinazojishughulisha na masuala ya hifadhi ya Mazingira zilizoko katika Bonde la Ziwa Nyasa.

Mradi mwingine ni ule wa Kujenga uwezo wa jamii za Pwani kuhimili mabadiliko ya tabianchi ili Kuwezesha jamii za pwani kuhimili mabadiliko ya tabianchi hasa yale yanayotokana na kuongezeka kwa kina cha bahari. Kupitia mradi huu mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi yametolewa kwa wataalam zaidi ya (80) wa Halmashauri za wilaya ya Rufiji, Pangani, Bagamoyo pamoja na Zanzibar; umepanda hekta 1,032 za mikoko (Rufiji 792 na Zanzibar 240) kati ya 1250 (Rufiji 1000, Zanzibar 240 na Pangani 10) zilizopangwa kupandwa, na kuandaa vitalu vya miche ya mikoko vinne (4) (Pangani 3 (miche 21,000) na Zanzibar 2 (5000); umekamilisha ujenzi wa ukuta wa Kisiwa Panza-Pemba wa mita 40,  unajenga ukuta wa Pangani kwa mita 550, ambapo asilimia 30 imeshajengwa, na unajenga makinga bahari  Kilimani-Unguja katika mita 538 ili kuzuia mmomonyoko wa fukwe za bahari katika maeneo hayo. Mradi pia umeanza kazi ya uchimbaji visima 10 na ujenzi wa mifumo ya kuvuna maji ya mvua miwili (2) katika Wilaya ya Bagamoyo ili kukabiliana na kuingia maji ya chumvi katika visima vya zamani. Ni faraja kubwa kwa wakazi wa Pwani ambao kwa kiasi kikubwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ilikuwa ni changamoto kubwa kwao.

Miradi mingine inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ni pamoja na Mradi wa Kukabiliana na Kasi ya Uharibifu wa Ardhi na Kuongeza Upatikanaji wa Chakula katika Maeneo Kame Nchini (Reversing Land Degradation Trends and Increasing Food Security in Degraded Ecosystems of Semi-arid areas of Tanzania, wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 7.1, Mradi Kuhimili mabadiliko ya Tabianchi katika Mifumo-ikolojia ya maeneo ya Vijijini (Ecosystem Based Adaptation for Rural Resilleience), wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7.57. Utekelezaji utafanyika kwa kushirikiana na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (United Nations Environment Programme – UNEP). Tukiwa waratibu na wasimamizi wa Mazingira Nchini Ofisi ya Makamu wa Rais imeratibu upatikanaji wa fedha kutoka Green Climate Fund na mifuko mingine ya  Mazingira. Mpaka sasa Ofisi imewezesha upatikanaji wa  Dola za Marekani milioni 140   (USD milioni 100 Simiyu kupitia KfW na takriban   USD 40 milioni  kupitia  Tanzania Private Sector Foundation) kutoka Mfuko wa dunia wa mabadiliko ya tabianchi  (Green  Climate Fund)  kwa ajili ya upatikanaji wa maji Simiyu.

Ofisi ya Makamu wa Rais tutaendelea na juhui za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama kwa mustakabali wa wananchi wetu na kuhakikisha Muungano unalindwa na kudumishwa kwa manufaa yetu sote.