HATUTAONGEZA MUDA MARUFUKU YA MIFUKO YA PLASTIKI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba amesema kuwa Ofisi yake kamwe haitarudi nyuma kusimamia katazo la matumizi ya mifuko ya Plastiki ifikapo Juni Mosi mwaka huu ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakilalamika kuwa kipindi kilichotolewa ni kifupi.

Akizindua program maalumu ya kuelemisha umma juu ya “Marufuku ya Mifuko ya Plastiki nchini” Waziri Makamba amesema kuwa Kanuni zimeweka bayana aina ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufu na kuainishi aina za tozo na adhabu mbalimbali zitakazotolewa kwa kila kosa. “Tumepiga marufuku uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini” hata hivyo kuna vifungashio ambavyo havitahusika na katazo hili mfano; vifungashio vya pembejeo za kilimo, madawa na baadhi ya vyakula.

Amesema agizo hili limekuwa shirikishi na kusisitiza kuwa wadau wote muhimu walishirikishwa ikiwa ni pamoja na wenye viwanda na wazalishaji wa mifuko mbadala. “Shirikisho la wenye viwanda waliniandikia barua na kuomba katazo la matumizi ya mifuko hii ya plastiki lianze kutumika mwezi Desema 2017, Serikali imetekeleza maombi haya mwaka mmoja baadae, sasa iweje watu walalamike kuwa muda hautoshi?” alihoji Waziri Makamba.

Waziri Makamba amewata wawekezaji kutumia fursa ya kuwekeza katika uzalishali wa mifuko mbadala na kusisitiza kuwa kuwa kupitia kikao na Wazalishaji wa Mifuko mbadala wa plastiki kilichofanyika mapema mwezi huu wazalishaji wa mifuko mbadala wamethibitisha kuwa mbadala wa plastiki upo kwa kiasi cha kutosha.

Amesema wafanya biashara wenye mzigo/shehena kubwa ya mifuko ya plastiki wajitokeze ili Serikali iweke mazingira rafiki ya kuwezesha kuuza bidhaa hizo katika Nchi na mataifa mbalimbali ambako bidhaa hiyo itahitajika.

Aidha, Waziri Makamba ametoa onyo kwa ‘viwanda bubu’ ambavyo vimeendelea kuzalisha mifuko hiyo iliyopigwa marufuku na kusisitiza kuwa msako unaendelea.

Waziri Makamba amesisitiza kuwa Serikali imeunda kikosi kazi kitakachoratibu utekelezaji wa zoezi hili kikosi kazi kinachojumuisha watendaji kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Shirika la Viwango Tanzania. Wengine ni Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Aprili 9 mwaka huu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alitangaza Juni Mosi 2019 kuwa mwisho wa matumizi ya Mifuko ya Plastiki hapa nchini.