ZIWA SINGIDANI MBIONI KUTANGAZWA ENEO LINDWA KIMAZINGIRA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba amesema Ofisi yake inaangalia uwezekano wa kutangaza Ziwa Singidani na Ziwa Kindai katika Halmashauri ya Singida kama maeneo lindwa kimazingira kwa kuwa yako hatarini kutoweka.

Waziri Makamba ameyasema hayo hii leo Mkoani Singida ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake katika Mikoa 9 hapa nchini yenye lengo kukagua, kutathmini na kuzungumza na viongozi, wataalam, watendaji na wananchi kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira  kifungu namba 51.

Aidha, Waziri Makamba amesema kuwa mara baada ya kutoa tangazo hilo katika gazeti la Serikali matumizi sahihi ya maziwa hayo yataainishwa ikiwa ni pamoja na kupanda miti rafiki kuzunguka maeneo yote na kuzingatia makatazo yatakayotolewa.

“Ziwa Singidani liko hatarini kutoweka kutona na shughuli za kibinadamu, hivyo kwa kutumia Sheria ya Mazingira nitashauriana na wataalamu wangu kuona namna bora ya kunusuru maziwa haya ikiwa ni pamoja na kuyatangaza kwenye gazeti la Serikali kama maeneo lindwa kimazingira.” Makamba alisisitiza.

Imebainika kuwa, lengo la kuainisha na kutangaza maeneo hayo ni kulinda mifumo muhimu ya kiikolojia (ikiwemo vyanzo vya maji, mito, maziwa, mabwawa, milima na vilima, chemichemi, ardhi oevu, mazalia ya samaki na misitu) ambayo hayana ulinzi wa Sheria nyingine.

Waziri Makamba pia ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Singida kwa utayari na uwezo wao katika kusimamia uhifadhi mara maeneo hayo yatakapotangazwa na kuwataka kuwasiliana na Ofisi yake ili waweze kupatiwa rasimu ya Sheria ndogo ndogo watakazozitumia katika Halmashauri zao ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira katika ngazi zote.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema Mkoa wake uko tayari kuingia makubaliano na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yenye lengo la kuhuisha Sheria ndogo ndogo zitakazosaidia hifadhi ya Mazingira mkoani kwake pamoja na kuundwa kwa  Kamati za Mazingira katika ngazi zote.

Jumla ya maeneo 77 yamependekezwa kutoka Mikoa mbalimbali kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria na katika awamu ya kwanza, maeneo takriban 20 yanatarajiwa kuhifadhiwa kwa kutumia Sheria ya Mazingira.