Waziri Simbachawene atoa wito kutangaza mazuri ya Muungano

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mhe. George Simbachawene amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa kipekee na kuwataka Watanzania kutangaza faida na mafanikio yake.

Ametoa kauli hiyo Agosti 5, 2019 wakati wa ziara yake Zanzibar wakati wa kujitambulisha kwa viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waziri Simbachawene alisema kuwa Muungano wetu unaishi na kukabiliana na changamoto mbalimbali hata hivyo changamoto hizo haziwezi kuzidi mafanikio yaliyotokana na Muungano wetu.

Kwa mantiki hii, hatuna budi kujivunia na kuyatangaza mambo mazuri lukuki yaliyotokana na Muungano huu kuliko kuzitangaza zaidi changamoto zinazoukabili MuMuungano.

Aidha, alisema anategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wataalam mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na yeye aliwahakikishia mchango wake wa mawazo katika kuutunza, kuulinda na kuuendeleza Muungano huu adhimu.

“Aliongeza kusema kuwa, sasa ni wakati wa kuhakikisha elimu sahihi ya Muungano inatolewa kwa kizazi kilichozaliwa baada ya Muungano ili kiweze kuelewa dhamira nzima ya kuasisiwa kwa Muungano kwani walio wengi wanasoma historia ya Muungano katika vitabu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud alisema Serikali hizi mbili zina jukumu la kuutunza na kuuendeleza Muungano.

Mhe. Mohamed Aboud alisema Ofisi hizi za Makamu wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais zinahitaji kufanya kazi kwa ukaribu na kuwa chachu ya kuhakikisha Muungano wetu unaimarika na kuendelea kuwa Muungano wa mfano Duniani kote.

“Nakukukaribisha sana Mheshimwa Waziri na milango ipo wazi tushirikiane kuimarisha Muungano wetu ili tutekeleze wajibu wetu wa kusimamia mambo ya Muungano,” alisema Mhe. Mohamed Aboud.