Waziri Makamba: Serikali kuhakikisha vyanzo Mto Rufiji vinalindwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema Serikali imejipanga kuhakikisha vyanzo vyote vya Mto Rufiji vinatunzwa na kulindwa wakati wote wa ujenzi wa mradi wa kufua umeme Stiegler’s Gorge.

Mhe. Makamba amesema hayo alipotembelea mradi huo uliopo katika maporomoko ya Mto Rufiji mkoani Pwani unaotekelezwa.

Alisema ziara hiyo imelenga kukagua maendeleo ya mradi huo na kuona masuala mahsusi ya kimazingira yanayopaswa kuzingatiwa.

“Ili mradi huu uwe endelevu unahitaji maji yapatikane kwa wingi ili yaweze kujaza bwawa lakini kupatikana kwa maji hayo kunategemea hifadhi ya mazingira eneo la catchment, maeneo ya juu mbali ambapo Mto Rufiji unaanzia,” alisisitiza.

Waziri Makamba alibainisha maeneo kama Njombe, Iringa na Mbeya hasa kwenye mito ya Kilombero, Luhwegu na Ruaha Mkuu ambayo inachangia kwa sehemu kubwa maji katika Mto Rufiji unaojaza bwawa kwenye mradi huu.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa ndiyo imebeba dhamana ya usimamizi wa hifadhi ya mazingira wajibu wake ni kuwezsha miradi mikubwa ya kitaifa kuhakikisha inazingatia uhifadhi wa mazingira.

Alisema tayari Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefungua Ofisi zake katika eneo hilo ili kusimamia kwa ukaribu masuala ya mazingira na kuwa mradi haukwami wala kusababisha athari kwa mazingira.