Article 1

HOTUBA YAMHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA, MWALIMU JULIUS NYERERE PAMOJA NA SHEREHE ZA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE NA WIKI YA VIJANA KITAIFA MKOANI MJINI MAGHARIBI, TAREHE 14 OKTOBA, 2017

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;

Mheshimiwa Moudline Cyrus Castico, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto wa Zanzibar;

Mheshimiwa Jenista Muhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;

Ndugu Mwakilishi wa Familia ya Baba wa Taifa, Mheshimiwa Makongoro Nyerere;

Mama Yetu Mpendwa, Mama Fatuma Karume;

Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri mliopo;

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na Wakuu wa Mikoa wote mliopo;

Mheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mkiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi;

Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mliopo;

Waheshimiwa Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

Ndugu Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu mliopo;

Waheshimiwa Viongozi wa Dini mliopo;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, ambaye ametuwezesha kukutana katika siku hii muhimu. Kama mnavyofahamu, Siku hii imebeba mambo makubwa mawili, au naweza kusema matatu. Kwanza, tunakumbuka kifo cha Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye tarehe kama ya leo, miaka 18 iliyopita, alitutoka hapa duniani. Na Pili, kulingana na maelekezo ya Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 11 wa Mwaka 2002, Siku ya leo pia ni kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu na Wiki ya Vijana Kitaifa.

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri husika kwa kunialika kwenye shughuli hii muhimu. Kama mnavyofahamu, hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki kwenye shughuli hii tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Mwaka jana, sherehe hizi zilipofanyika kule Simiyu, nilimwomba Mheshimiwa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein Rais wa Serikali ya Zanzibar aniwakilishe, ambapo alifanya kazi hiyo vizuri sana huko Bariadi. Hivyo, kwa hakika kabisa, nimefurahi sana kushiriki kwenye shughuli hii.

Nitumie pia fursa hii kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Zanzibar kwa ujumla kwa mapokezi yenu mazuri. Aidha, nawashukuru kwa kujitokeza kwenu kwa wingi katika shughuli hii. Kama msemo wa Kiswahili usemavyo ”shughuli ni watu”. Hivyo, nasema, ahsanteni sana.

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kama nilivyotangulia kusema, moja ya mambo yaliyotukutanisha hapa leo ni kukumbuka kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambacho kilitokea London, Uingereza, siku kama ya leo mwaka 1999. Tangu wakati huo, kila mwaka, ifikapo tarehe 14 Oktoba, tunafanya maadhimisho haya. Tutafanya hivyo pia mwakani na naamini tutafanya hivyo kwa miaka mingi ijayo kama si katika kipindi chote cha uhai wa Taifa letu.

Lakini, Watanzania wenzangu, tujiulize, hivi ni kwanini hasa tunamkumbuka Mwalimu Nyerere? Je, ni kwa sababu tu Siku hii imetamkwa kwenye sheria? Au tuna sababu za msingi za kumkumbuka? Tusipojiuliza maswali hayo, tutaendelea kuiadhimisha Siku hii kwa mazoea na hatimaye itapoteza umuhimu wake. Lakini niseme tu kuwa, nijuavyo mimi ni kwamba, Siku hii iliamriwa kuwa Siku ya Kitaifa ili kuwapa Watanzania fursa ya kujikumbusha mchango mkubwa na usiosahaulika uliotolewa na Mwalimu Nyerere katika nchi yetu. Na katika kujikumbusha huko, tujifunze na kutumia mafunzo tunayoyapata katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu.

Mabibi na Mabwana;

Nafahamu kuwa Watanzania wengi wanamfahamu au wamewahi kusikia habari za Mwalimu Nyerere. Baadhi walishiriki naye katika shughuli mbalimbali. Wengine walimuona wakati akiwa Rais. Wapo pia waliomfahamu kupitia vitabu au simulizi mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa siku hii, na kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kushiriki kwenye maadhimisho haya tangu niwe Rais, nimeona ni jambo jema kumzungumzia kidogo Mwalimu Nyerere. Hii ni kwa sababu, sisi wenyewe, lakini hasa vijana na watoto wetu, wanahitaji kumfahamu vizuri mtu huyu tunayemkumbuka leo na pia kufahamu kwa nini tunafanya hivyo.

Ndugu Watanzania, Mabibi na Mabwana;

Historia ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ni ndefu sana. Lakini niseme tu kuwa tunamkumbuka kwa sababu, kwanza, alikuwa kiongozi mzalendo. Mwalimu Nyerere alianza uongozi wa kisiasa mwaka 1953 alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika African Association (TAA). TAA ndio iliyozaa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho ndicho kilichoongoza harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu.

Katika kipindi hicho cha mwanzoni kabisa cha uongozi wake kisiasa, Mwalimu Nyerere alionesha uzalendo wa hali ya juu na kuthamini kwake utu na usawa wa binadamu. Wakati anachaguliwa kuwa Rais wa TAA na baadaye TANU, alikuwa anafundisha St.Francis College, hivi sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari Pugu. Umbali wa kutoka Pugu hadi kwenye Ofisi za TAA/TANU kwenda na kurudi ilikuwa kama kilometa 46. Na enzi hizo hapakuwa na usafiri wa daladala kama ilivyo sasa. TAA/TANU haikuwa na usafiri na hata fedha za kumlipa mshahara. Lakini kwa uzalendo wake, Mwalimu Nyerere alitumia fedha zake kujigharamia usafiri na wakati mwingine kulazimika kutembea kwa miguu. Alifanya hivyo kwa kujitolea. Tujiulize leo, ni viongozi wangapi wa Serikali na hata kwenye vyama wameweza kujitolea kiasi hicho?

Lakini kama hiyo haitoshi, mwaka 1955, alipotakiwa na Mwalimu Mkuu wa St.Francis College kuchagua ama kuendelea na kazi au kuacha kujihusisha na shughuli za kisiasa, Mwalimu Nyerere aliamua kuacha kazi na kubaki kuwa kiongozi wa TANU; kazi ambayo alikuwa halipwi mshahara wowote. Aliamua hivyo ili aendelee kuongoza harakati za kudai uhuru. Sijui kama tunafahamu maisha aliyoishi Mwalimu Nyerere na familia yake baada ya kuacha kazi; lakini, nina uhakika, yalikuwa magumu sana.

Kitu pekee kilichomsukuma kufanya uamuzi huo ni uzalendo wake. Isingekuwa hivyo, angetafuta kazi nyingine nzuri ya mshahara mzuri, kwa maana alikuwa msomi mzuri; na wasomi wa kiwango chake, wakati huo walikuwa wakihitajika sana. Je, tujiulize ni wangapi hivi leo wanaweza kufanya uamuzi wa kizalendo kama huo uliofanywa na Baba wa Taifa? Leo hii kuna Watanzania wangapi ambao kwa sababu tu wanalipwa vizuri kwenye makampuni ya wageni wanakofanya kazi, wanaisaliti nchi kwa vitendo vya wizi? Je, kuna viongozi wangapi waliopewa dhamana na wananchi lakini kwa sababu ya ubinafsi na kukosa uzalendo, wamekubali kusaini mikataba isiyo na tija kwa nchi? Je, tuna viongozi wangapi ambao wametanguliza maslahi yao binafsi mbele kuliko maslahi ya Tanzania? Majibu mnayo.

Ndugu Watanzania, Mabibi na Mabwana;

Sifa ya pili ya Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi asiye mbinafsi na mwenye kuthamini utu na usawa wa binadamu. Hili linadhihirishwa kwa jinsi yeye na familia yake walivyoishi. Waliishi maisha ya kawaida sana kama Watanzania wengine. Hakujilimbikizia mali wala hakuishi maisha ya anasa na kifahari. Kuna mtu niliwahi kumsikia akisema”kama Mwalimu Nyerere angekuwa mbinafsi au mpenda utajiri angeweza kuchukua fukwe yote ya Msasani ili iwe yake”. Na kweli angeweza, maana kuna mifano mingi tu ya viongozi wengi wa zama zake, na hata wa sasa, wanafanya hivyo. Lakini hakufanya hivyo. Yeye, Mama Maria, watoto na ndugu zake wengi waliishi na wanaendelea kuishi maisha ya kawaida kabisa, sawa na Watanzania wengi, licha ya kuwa Rais kwa takriban miaka 23.

Mfano mwingine unaodhihirisha kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa mbinafsi bali mwenye kuthamini utu na usawa wa binadamu, ni jambo alilolifanya mwanzoni tu mwa uongozi wake akiwa Rais wa Tanzania. Baada ya nchi yetu kupata uhuru, baadhi ya wasomi waliokabidhiwa madaraka walianza kutoa shinikizo kwa Serikali kutaka kuongezewa mishahara na marupurupu. Mwalimu Nyerere hakukubaliana kabisa na madai hayo na hakusita kuikemea tabia hiyo ya ubinafsi kwa ukali na uwazi kabisa.

Hakuishia hapo. Ili kuonesha mfano, yeye mwenyewe, aliamua kupunguza mshahara wake ili kuwakumbusha wasomi hao kuwa haiwezekani kwa watu wachache kuongezana mishahara wakati wananchi wengi masikini hawapati huduma muhimu za afya, elimu na maji kutokana na ukosefu wa fedha. Tujiulize, je, sisi tuko tayari kuacha mishahara hewa? Je, mishahara tunayoipata tunaifanyia kazi? Je,nasi tupo tayari kujipunguzia, au kuacha kushinikiza kuongezwa kwa mishahara na marupurupu yetu ili kuiwezesha Serikali kuboresha huduma za jamii kwa manufaa ya Watanzania wote? Nasema hayo sio kwa sababu sitaki mishahara iongezwe. La hasha. Ninachotaka kusema ni kwamba kabla ya kudai nyongeza ya mishahara ni lazima kwanza kufahamu uwezo wa Serikali; lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanaohitaji kuboreshewa huduma.

Nafahamu kuwa huku Zanzibar mishahara ya watumishi wa kima cha chini imeongezwa kutoka Shilingi laki moja na nusu hadi shilingi laki tatu. Na kwa upande wa kule Bara, baada ya kukamilisha zoezi la uchambuzi wa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi, Serikali imewapandisha vyeo watumishi 59,967 na kurekebisha mishahara yao, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 159.33 kimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu. Mishahara mipya ya watumishi hao inatarajiwa kuanza kulipwa mwezi huu. Endapo tusingefanya uchambuzi, Serikali ingepoteza takriban shilingi bilioni 89 kwa mwaka kwa kuwalipa watumishi hewa na wenye vyeti feki.

Ndugu Watanzania, Mabibi na Mabwana;

Sifa nyingine ya Mwalimu Nyerere alikuwa mpenda amani, umoja na mshikamano. Wakati wa harakati za kudai uhuru, aliwahimiza Watanganyika kutotumia nguvu, licha ya kuwepo kwa vitendo vya uchokozi na hila chafu zilizofanywa na wakoloni. Hii ndio moja ya sababu, zilifanya nchi yetu kupata uhuru kwa njia ya amani. Aidha, licha ya kuwa Tanganyika ilikuwa na takriban makabila 121 na dini mbalimbali, alifanikiwa kuwaunganisha wananchi wote katika harakati za kudai uhuru wa nchi yao.

Mwalimu Nyerere pia alikuwa muumini mzuri wa Muungano. Tanganyika ilipokaribia kupata uhuru, alikuwa tayari kuchelewesha uhuru huo kuzisubiri nchi nyingine za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda na Zanzibar) ili uhuru huo upatikane kwa pamoja na kuwezesha kuundwa kwa taifa moja la Shirikisho la Afrika Mashariki. Lakini hata pale ilipodhihirika kuwa suala hilo haliwezekani, mwaka 1964, Baba wa Taifa pamoja na shujaa mwingine wa nchi yetu, Hayati Mzee Abeid Aman Karume, waliasisi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Na mwaka 1977, viongozi hao waliasisi Muungano wa vyama vya TANU na Afro Shiraz Party, na kuunda CCM, Chama Tawala, ambacho kimebaki kuwa miongoni mwa vyama vikongwe duniani. Hii inadhihirisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mpenda muungano. Tujiulize je, vitendo vyetu leo vinalenga kudumisha amani ya nchi yetu au kuivunja? Je, sisi hatuna udini au ukabila? Je, maneno na vitendo vyetu vinadumisha au vinahatarisha Muungano wetu? Haya ni maswali muhimu kujiuliza Watanzania wote tunapoadhimisha siku hii ya Mwalimu Nyerere.

Wheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Kiongozi yoyote ana sifa kubwa moja; kuwa na maono (vision). Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye maono, tena makubwa na ya mbali sana. Alijua kuwa anataka kujenga Taifa huru na linalojitegemea. Taifa la watu wenye kujali na kuheshimu utu wa kila mmoja. Hayo ndio maono yake. Lakini, kama mnavyofahamu, maono peke yake bila mikakati, ni ndoto. Mwalimu Nyerere alibuni na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kutekeleza maono yake. Ndani ya miaka michache tu baada ya nchi yetu kupata uhuru, Mwalimu Nyerere alibaini kuwa huwezi kujenga Taifa huru na linalojitegemea kama njia kuu za uzalishaji zitamilikiwa au kusimamiwa na wageni au watu binafsi peke yake. Ni lazima Serikali ishiriki kikamilifu. Na huo ndio ukweli wenyewe. Nchi zote zilizofanikiwa kiuchumi duniani, Serikali zao zilishiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi. Hivyo basi, aliona upo umuhimu wa kujenga misingi itakayoiwezesha Serikali kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji; na hapo ndipo Azimio la Arusha likazaliwa mwaka 1967.

Mbali kuweka miiko ya kuwabana viongozi kutumia nafasi zao kujilimbikizia mali, Azimio la Arusha liliipa nguvu Serikali ya kuzuia viwanda, mashirika na makampuni ya kibepari kutorosha rasilimali zetu kwenda nje ya nchi. Lakini pia, kupitia Azimio la Arusha, Serikali ilijenga viwanda pamoja na kuanzisha mashirika na makampuni mengine mapya. Tukawa na viwanda vingi tu, vikiwemo vya nguo, viatu, matairi, vifaa vya kilimo, chuma, n.k.; na hivyo tukapunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa hizo kutoka nje. Shirika letu la ndege lilikuwa na uwezo wa kutoa huduma ndani na nje ya nchi. Nakumbuka tulikuwa na ndege 9; mbili aina ya Boeing, Fokker 3 na Twin Otters 4. Aidha, Serikali ikaanzisha Shirika la Nyumba (NHC), ambalo lilikuwa na nyumba zipatazo 6,000 kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini. Na huku Zanzibar, Hayati Mzee Karume, akajenga majengo ya ghorofa sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na pale Michenzani.

Sambamba na hayo, Serikali iliweka mkazo kwenye elimu, ambapo ilitolewa bure bila ubaguzi, kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa ukitaka kumkomboa mtu mnyonge ni lazima umpe elimu. Vilevile, alihimiza watu kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia kaulimbiu za “uhuru na kazi”, “siasa ni kilimo”, n.k. Hii ni baadhi tu ya mikakati iliyotumiwa na Mwalimu Nyerere katika kujenga Tanzania aliyotaka. Lakini pia, kwa kutambua hali halisi ya nchi yetu wakati huo, Baba wa Taifa, aliwahi kutamka, nanukuu “madini yetu tuliyonayo ni vema tukayaacha mpaka Watanzania watakapokuwa na ufahamu wa kutosha wataamua kuyachimba”, mwisho wa kunukuu.

Pamoja na misingi hiyo mizuri iliyowekwa na Baba wa Taifa, kupitia Azimio la Arusha, miaka michache tu baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka Azimio la Arusha lilikatupwa. Sasa sijui ilitokea kwa makusudi au bahati mbaya. Mimi sijui, ila ukweli ni kwamba, tulilitupa. Na baada ya kulitupa tukaanza kuuza mashirika na viwanda vyetu, hata vile vilivyojiendesha kwa faida, kwa matarajio kwamba tutakaowauzia wangeviendesha kwa ufanisi zaidi. Lakini haikuwa hivyo. Viwanda na mashirika mengi tuliyoyabinafsisha, sasa yamekufa. Leo viko wapi viwanda vya nguo, ngozi, nyama, matairi n.k? Kwa takwimu nilizonazo, jumla ya viwanda 197 vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere hivi sasa havipo; vimekufa. Na hapa ndipo mara nyingi mimi huwa najiuliza, ni nani hasa aliyeturoga sisi Watanzania? Kwa nini tuliamua kuuza viwanda vyetu? Ilikuwaje tukaruhusu Shirika letu la Ndege libaki na ndege moja kutoka 9 zilizokuwepo? Kwanini Shirika letu la Nyumba lishindwe kujenga nyumba za wananchi wa kipato cha chini? Hivi wananchi wana namna hiyo hivi sasa hawapo? Au hawahitaji tena makazi mazuri na ya gharama nafuu? Lakini swali kubwa ninalojiuliza kila wakati ni kwanini tuliliacha Azimio la Arusha wakati maudhui na misingi yake, binafsi, mpaka leo, naiona kuwa ni mizuri. Ndio, ni mizuri. Tunachoweza kujadiliana ni kuhusu mikakati ya utekelezaji wake kwa nyakati za sasa, lakini maudhui na misingi yake bado ni mizuri.

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jitihada za Baba wa Taifa kutetea wanyonge, kupigania umoja, amani, haki na usawa, hazikuishia tu hapa nchini. Zilivuka hadi nje ya mipaka ya nchi yetu. Tanzania, chini ya uongozi wa Mwalimu, ilikuwa mstari wa mbele kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika. Ilikuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya OAU; na pia ilitoa hifadhi na mafunzo kwa vyama vya ukombozi vya Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe, hadi nchi hizo zilipopata uhuru. Kama hiyo haitoshi, jana niliongea na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye aliniambia kuwa bila Mwalimu Nyerere huenda yeye asingekuwa Rais wa Uganda hivi sasa.

Mbali na kutoa mchango kwenye harakati za ukombozi, Baba wa Taifa alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa OAU, sasa Umoja wa Afrika, na pia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Tanzania pia chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, ilikuwa mtetezi wa haki za wanyonge duniani kote. Mathalan, tulikuwa mstari wa mbele kutetea haki ya Jamhuri ya Watu wa China kupata uanachama kwenye Umoja wa Mataifa. Zaidi ya hapo, Mwalimu Nyerere alishiriki kwenye usuluhishi wa migogoro Barani Afrika. Na katika kudhihirisha hilo, wakati anafariki alikuwa Msuluhishi wa mgogoro wa Burundi.

Huyo ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Mpigania Uhuru; Mwanafrika halisi (Pan-Africanist); Mpenda Amani, Haki, Umoja na Usawa; Rais wa TAA na TANU; Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika; Rais wa Jamhuri ya Tanganyika; Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mwenyekiti wa kwanza wa CCM; Baba wa Taifa letu, ambaye leo tunakumbuka kifo chake na kusheherekea maisha yake. Kwa ujumla, naweza kusema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa miongoni mwa viongozi bora kuwahi kutokea sio tu hapa nchini, bali pia Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Vijana na watoto wetu hawana budi kumfahamu mtu huyu wa aina yake katika historia ya nchi. Tuwafundishe watoto wetu fikra za Mwalimu Nyerere. Tuwasimulie kazi na mambo aliyoyasimamia. Na Watanzania wote kwa ujumla, hatuna budi kuenzi mambo mazuri aliyotuachia Baba wa Taifa letu. Nyerere oyeeee!!!!!

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Hayo niliyoeleza na maswali niliyouliza lengo lake sio kumtuhumu mtu yeyote. Nimeeleza na kuuliza maswali hayo kwa lengo la kumpa kila Mtanzania, fursa ya kutafakari ili kubaini wapi tulijikwaa au kukosea; na hatimaye tutafute njia ya kujisahihisha. Ni wazi kuwa, Baba wa Taifa, kama binadamu, alikuwa na mapungufu yake. Hata hivyo, mimi naamini kuwa endapo kila Mtanzania ataamua kwa dhati ya moyo wake kuenzi mambo mazuri ya Mwalimu Nyerere, nchi yetu itapata maendeleo makubwa tena kwa haraka.

Na katika hili, napenda nitumie fursa hii kuwathibitishia, kwa niaba ya mwenzangu Mheshimiwa Rais Shein, kuwa Serikali zetu mbili zimejipanga kuhakikisha zinaendelea kusimamia masuala na misingi mizuri iliyoachwa na waasisi wetu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, pamoja na viongozi waliofuata wa nchi yetu. Ni dhahiri kuwa kuvaa viatu vyao sio jambo rahisi. Lakini, nina imani kuwa, kwa ushirikiano wenu, tutaweza kuyasimamia na kuyatekeleza haya. Mathalan, moja ya ndoto za Baba wa Taifa ilikuwa kuhamishia Makao Makuu ya nchi yetu, Dodoma. Uamuzi wa kuhamia Dodoma ulifanyika tangu mwaka 1973, lakini utekelezaji wake ulikuwa ukilegalega kwa sababu mbalimbali. Sisi tumeamua kuhamia Dodoma. Na tayari tumeshaanza kuhamia huko. Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya watendaji kutoka Wizara zote tayari wameshamia. Waziri Mkuu naye amehamia. Makamu wa Rais atahamia mwaka huu; na mimi nitahamia mwakani. Hii inadhihirisha kuwa tumedhamiria kwa dhati kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo na siyo maneno.

Sambamba na hilo, Serikali zetu mbili zitaendelea kuimarisha Umoja, Mshikamano na Muungano wetu. Tutadumisha pia amani yetu. Yeyote atakayejaribu kuhujumu Muungano wetu au kuvuruga amani yetu, tutapambana naye kwa nguvu zetu zote; na kwa vyovyote vile, atambue kuwa kamwe hatoshinda.

Zaidi ya hapo, tutaendeleza harakati za kujiletea maendeleo ya kiuchumi. Tutaimarisha na kuboresha miundombinu muhimu ya kiuchumi, hususan ya usafiri na nishati. Na katika hili, tumeamua kwa dhati kabisa kufufua Shirika letu la Ndege, ambalo kama nilivyoeleza awali, wakati wa Baba wa Taifa lilikuwa likifanya vizuri sana. Tayari tumenunua ndege mpya sita; mbili tayari zimewasili na zinatoa huduma. Na zile nyingine, napenda niwahakikishie kuwa nazo zitakuja. Aidha, tumeamua kutekeleza mradi mkubwa wa umeme wa Stiglier’s Gorge, ambao nao ulibuniwa tangu enzi za Baba wa Taifa. Sisi tumeamua kuutekeleza. Mradi huu utakapokamilika utazalisha takriban Megawati 2,100. Tumeshatangaza zabuni; na nimearifiwa kuwa makampuni 79 yamejitokeza kuomba zabuni ya kujenga mradi huo.

Tutaendelea kupanua wigo na kuboresha huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji. Kwa bahati nzuri, Serikali zetu mbili kila mwaka zimekuwa zikiongeza bajeti kwenye sekta hizo. Aidha, tutaimarisha usimamizi wa rasilimali zetu. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ina rasilimali nyingi: madini, mafuta, gesi, misitu, maeneo ya hifadhi na wanyamapori, pamoja na rasilimali za kwenye bahari, maziwa na mito. Lakini ninyi ni mashahidi, rasilimali hizi bado hazijatunufaisha. Ni watu wachache tu humu nchini na wengine kutoka nje, ndio wenye kunufaika nazo.

Napenda kuwaahidi kuwa katika kipindi changu cha uongozi, kamwe sitaruhusu hali hiyo kundelea. Nitashirikiana na mwenzangu Rais Shein pamoja na ninyi wananchi katika kuhakikisha rasilimali zetu zinatunufaisha. Tayari tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali. Kule Bara, kwa mfano, mwezi Julai mwaka huu, tulishapitisha sheria ya kulinda rasilimali zetu, hususan madini. Aidha, tumedhibiti biashara ya madini; na matokeo yake tumeanza kuyaona. Mathalan, kufuatia agizo langu nililolitoa mwezi Machi, 2017 kuhusu kuimarisha usimamizi wa rasilimali zetu, hususan madini, uzalishaji umeongezeka tofauti na tulivyokuwa tukiambiwa awali. Nitatoa mifano michache. Kabla ya agizo langu, almasi iliyozalishwa mwezi Januari 2017, ilikuwa carats 18,808.1; Februari 2017 carats 11,260.8; na mwezi Machi 2017 carats 15,743. Na niaka ya nyuma nayo, hali ilikuwa ni hivyo. Lakini baada ya agizo, uzalishaji umeongezeka. Mwezi Juni 2017 tulizalisha carats 28,889.7; mwezi Julai 2017 carats 27,578.75; Agosti 2017 carats 32,753; na Septemba 2017 carats 27,578.75. Na sio almasi pekee ndio uzalishaji umeongezeka. Uzalishaji wa Tanzanite piaumeongezeka.

Huu ni mwanzo tu. Tutachukua hatua hizi tulizozianza kwenye rasilimali zetu zote, ikiwemo gesi, utalii, misitu na baharini; ambako pia tumekuwa tukiibiwa sana. Na kuhusu rasilimali za maji, tayari tumeshaunda Chombo cha kusimamia uvuvi kwenye Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority), ambacho kwa bahati nzuri Makao Makuu yake yapo huku Zanzibar.

Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana;

Nafahamu kuwa kutokana na hatua tunazozichukua, wamejitokeza baadhi ya watu wanaowapotosha wananchi kwa kuwaambia kuwa hali ya uchumi wetu inadorora. Huo ni uzushi. Ukweli ni kwamba uchumi wetu unazidi kuimarika. Mwaka huu unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1, na hivyo kuifanya nchi yetu kushika nafasi ya tatu Barani Afrika. Sambamba na hilo, mfumuko wa bei unazidi kupungua. Mwezi Julai, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 5.2, lakini mwezi Agosti ulishuka hadi kufikia asilimia 5.0. Na matokeo yanaonekana. Bei za bidhaa nyingi zimeshuka. Mathalan, mfuko mmoja wa saruji hivi sasa unauzwa kwa wastani wa shilingi 10,500 kutoka wastani wa shilingi 15,000; mafuta ya kupikia yameshuka kutoka wastani wa shilingi 3,095 kwa lita hadi shilingi 2,863; mafuta ya taa yameshuka kutoka wastani wa shilingi 2,862 kwa lita hadi shilingi 1,925. Mifano ipo mingi.

Kama hiyo haitoshi, ujenzi wa viwanda unaendelea vizuri. Nafahamu kuna watu wanaobeza kuhusu ujenzi wa viwanda; lakini kweli ni kwamba vinajengwa. Mathalan, mwaka 2015 vilikuwepo viwanda 49,243, lakini hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka huu, vimeongezeka hadi kufikia viwanda 52,549. Hii inamaanisha kwamba tangu tumeingia madarakani vimejengwa viwanda vipya 3,306. Halikadhalika, uwekezaji unazidi kuongezeka. Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Duniani (World Investment Report) ya mwaka 2017 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Biashara na Maendeleo (UNACTAD), mwaka 2016 nchi yetu ilisajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.35, na hivyo kuongoza katika eneo letu la Afrika Mashariki. Aidha, kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, tulikuwa tumesajili miradi 271 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.496 itakayotoa ajira zipatazo 22,000. Hii inadhihirisha kuwa uchumi wa nchi yetu unakwenda vizuri.

Licha ya ukweli huo, natambua kuwa, kutokana na hatua tunazozichukua za kuwabana mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma, wapo wananchi wa kawaida kabisa, ambao sio wezi wala mafisadi, wanaothirika. Chukua mfano, umemkamata mwizi wa fedha za umma. Mwizi huyo kama alikuwa anatumia fedha alizoziiba kujenga nyumba zake, ni lazima ujenzi wa nyumba hizo utasimama. Ujenzi ukisimama, atakayeathirika sio huyo mwizi pekee, bali wajenzi waliokuwa wakijenga nyumba, mama lishe waliokuwa wakiwapikia wajenzi, bodaboda waliokuwa wakiwabeba wajenzi, wauza maji, soda n.k. Hili nalifahamu. Lakini kama kweli tunataka kupambana na wizi na ubadhirifu pamoja na kuleta maendeleo kwa nchi yetu, athari hizi hatuwezi kuzikwepa. Mabadiliko ya aina yoyote ile, lazima yana athari kama hizi. Lakini jambo la kututia moyo ni kwamba, athari hizi mara nyingi huwa ni za kipindi kifupi. Baada ya muda, zinakwisha. Kuna usemi usemao “Mabadiliko ni magumu mwanzoni, yanakuwa machungu yanapofikia katikati, lakini mwishoni matokeo yake ni mazuri na matamu”.

Hivyo, nawaomba wananchi mtuvumilie katika kipindi hiki cha mpito. Baada ya muda mfupi, mambo yatakuwa mazuri. Lakini hata kama hayatakuwa mazuri hivi karibuni, watoto na wajukuu wetu watanufaika. Na huo ndio uzalendo. Uzalendo maana yake ni kuwa tayari kujitolea kwa faida ya wengi au vizazi vijavyo. Waasisi na wazee wetu walifanya hivyo. Walijitolea kupigania uhuru wa nchi yetu, lakini tunaofaidi matunda ya uhuru ni sisi. Hivyo, na sisi hatuna budi kujitoa ili vizazi vyetu vijavyo vinufaike. Mimi pamoja na mwenzangu, Rais Shein, tumeamua kujitoa kuleta maendeleo ya nchi yetu. Hivyo, nawaomba wananchi mtuunge mkono. Je, mko tayari kutuunga mkono? Ahsanteni sana.

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Wageni Waalikwa;

Kama nilivyosema awali, Siku ya leo pia tunaadhimisha Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2017. Mwenge wa Uhuru ni moja ya tunu za nchi yetu, na uliasisiwa na Baba wa Taifa. Hata kabla ya nchi yetu kupata uhuru, Baba wa Taifa alitamka maneno yafuatayo katika Bunge la Kikoloni tarehe 22 Oktoba Mwaka 1959, nanukuu,”Sisi Watanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau”, mwisho wa kunukuu. Tamko hili, mbali na kuamsha zaidi hamasa na kuchochea harakati za nchi yetu kudai uhuru; lilibeba falsafa nzito inayotoa taswira ya Taifa ambalo Baba wa Taifa alitaka kulijenga: Taifa lenye amani, linalojitegemea na lenye kuheshimu misingi ya utu, haki na usawa wa binadamu.

Azma ya kuwasha Mwenge ilitimia kwenye mkesha wa Uhuru, tarehe 9 Desemba, 1961, ambapo marehemu Kapteni Alexander Nyirenda, na wenzake, waliupandisha Mwenge wa Uhuru katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Na tangu mwaka 1964, kila mwaka, Mwenge wa Uhuru umekuwa ukikimbizwa nchi nzima, kuzunguka Mikoa yote ya Tanzania Bara na huku Zanzibar, Halmashauri zote za Wilaya, Vijiji pamoja na Mitaa mbalimbali ili kuendelea kukumbushana misingi ambayo juu yake nchi yetu imejengwa na inaendelea kujengwa; na pia nafasi ya nchi yetu mbele ya mataifa na watu wa mataifa wengine.

Katika kukumbushana huku, mbio za Mwenge huambatana na shughuli za ujenzi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo shabaha yake ni kukuza utu na ustawi wa watanzania. Kila Mwaka, Mwenge huzindua miradi mbalimbali. Mathalan, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mwenge wa Uhuru umezindua jumla ya miradi 6,838 yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 2.51; wastani wa miradi 1,367.6 kwa mwaka, ambayo thamani yake kwa wastani ni shilingi milioni 500. Mwaka huu pekee (2017), miradi iliyozinduliwa ni 1,512 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1. Miradi ambayo imekuwa ikizinduliwa na Mwenge inahusu sekta za afya, elimu, kilimo, maji, mawasiliano, mazingira, ujenzi, uwezeshaji, uvuvi na viwanda.

Sambamba na hilo, kila mwaka, mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa na kaulimbiu yake, ambapo mwaka huu inasema“Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi Yetu”. Nawapongeza waliobuni kaulimbiu hiyo ambayo inakwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa letu na pia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa katika Mbio za Mwenge mwaka huu, jumla ya viwanda 148 vimeziduliwa. Viwanda hivyo vimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 468.46 na vinatarajiwa kuzalisha ajira 13,370. Pamoja na ajira hizo, nina uhakika kuwa viwanda hivyo vitaingizia nchi fedha za kigeni na kuipatia Serikali yetu mapato kupitia kodi; na hatimaye kusaidia kupunguza umaskini nchini. Hii ndiyo sababu tumekuwa tukihimiza ujenzi wa viwanda. Na hizi ni baadhi ya faida za Mwenge.

Watanzania Wenzangu;

Licha ya dhana na falsafa nzuri pamoja na faida za Mwenge nilizozitaja, wapo watu wanaoupinga na kutaka ufutwe. Mimi nawashangaa sana wanaosema ufutwe! Sijui ni watu wametokea sayari gani? Wakati mwingine huwa najiuliza hivi hawa nao kweli ni sehemu ya historia ya nchi hii? Najiuliza hivyo kwa sababu, kama kweli wewe ni Mtanzania na unaifahamu kidogo historia ya nchi hii pamoja na ya Baba wa Taifa na Mzee Karume, huwezi kuthubutu kutamka kuwa eti Mwenge ufutwe. Huwezi! Mwenge wa Uhuru ni tunu tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa hili. Na kamwe mimi siwezi kukubali Mwenge ufutwe. Niwaombe Watanzania wenzangu tuwapuuze, tuwazomee na kuwasuta wote wanaosema Mwenge ufutwe. Tunazo sababu nyingi za kukataa Mwenge wetu kufutwa, lakini kwa ajili ya muda, nitataja kama tatu hivi.

Kwanza, Mwenge wa Uhuru hautafutwa kwa sababu unachochea maendeleo. Kama mlivyosikia, wakati wa Mbio za Mwenge za Uhuru Mwaka huu, miradi mbalimbali ya maendeleo imezinduliwa. Natambua kuwa mojawapo ya hoja zinazotolewa na wenye kuupinga Mwenge wetu ni suala la gharama. Lakini mimi nafahamu kuwa katika mbio za Mwenge mwaka huu, Serikali ilitenga shilingi milioni 463 kugharamia. Sasa ukilinganisha kiasi hicho na miradi 1,512 iliyozinduliwa yenye thamani inayokaribia shilingi trilioni 1.1, ni dhahiri kuwa hoja ya gharama haina mashiko? Lakini nafahamu kuwa wapo watakaosema kuwa miradi hiyo ingeweza kuzinduliwa hata bila ya Mwenge. Huenda hilo ni kweli. Lakini tujiulize, je kama Mwenge usingekuwepo, viongozi wa vijiji, kata, tarafa, wilaya na hata mikoa kweli wangekuwa wanahagaika kila mwaka kubuni miradi, kama ilivyo sasa? Nadhani majibu mnayo.

Lakini ukiachilia mbali hilo, Mwenge wa Uhuru pia unatumika kufichua maovu. Hivi punde nimepokea taarifa ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, ambayo pamoja na masuala mengine, imefichua ubadhirifu kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi. Hii ndio kazi nyingine ya Mwenge wa Uhuru. Na napenda kutumia fursa kumhakikishia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali itafuatilia miradi hiyo na kuwachukulia hatua stahiki watakaohusika na ubadhirifu huo.

Pili, Mwenge wa Uhuru unawaunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano wetu. Kama nilivyogusia hapo awali, Mwenge wa Uhuru uzunguka nchi nzima, Tanzania Bara na Visiwani. Wanaokimbiza Mwenge wanatoka pande zote mbili za Muungano. Kwa kufanya hivyo, Mwenge unatuunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano wetu. Na kila unapopita mahali, unatoa matumaini mapya (kupitia miradi) na kusambaza upendo miongoni mwa Watanzania.

Tatu, na muhimu zaidi, ni kwamba Mwenge wa Uhuru ni alama ya uhuru na utaifa wetu. Kama mnavyofahamu, kila nchi hapa duniani ina alama zake za Taifa. Na sisi ni hivyo hivyo. Moja ya alama yetu ni Mwenge wa Uhuru. Nyingine ni Wimbo ya Taifa, Bendera ya Taifa, n.k. Hivyo kuufuta Mwenge wa Uhuru ni sawa na kufuta historia na alama inayotambulisha utaifa wetu.

Zaidi ya hapo ningependa kuwataarifu Watanzania wenzangu kuwa Mwenge au alama zinazofanana na Mwenge hazipo tu hapa nchini. Zipo nchi na taasisi za kimataifa zenye alama kama hii ya Mwenge wetu wa Uhuru. Baadhi ya nchi hizo ni majirani zetu wa Kenya, Msumbiji na Rwanda. Aidha, ninyi nyote hapa ni mashahidi, nchi yetu mara kadhaa imekuwa ikipokea Kifimbo cha Malkia wa Uingereza, Mwenge wa Olimpiki, Kombe la Dunia, n.k; lakini sijawahi, hata siku moja, kusikia watu wakipinga vifimbo hivyo kuja nchini au kutaka vifutwe. Sana sana tu, baadhi ya wanaoupinga Mwenge wetu, ndio hao hao wamekuwa mstari wa mbele kwenda kuvipokea vifimbo hivyo. Binafsi, siwapingi wao kwenda kupokea vifimbo hivyo. Acha waende, hakuna ubaya. Ubaya ni pale wanapoupinga Mwenge wetu, huku wakiona fahari kupokea vifimbo hivyo.

Hivyo basi, kwa niaba ya mwenzangu Mheshimiwa Rais Dkt. Shein, napenda kurudia tena kuwaambia watu hao kuwa, katika kipindi chetu cha uongozi, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuwepo. Na niwaombe Watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi yetu, mtuunge mkono.

Ndugu Viongozi,

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Jambo la tatu ambalo limetukutanisha hapa leo ni kuadhimisha kilele cha Siku ya Vijana Kitaifa. Kama mnavyofahamu, duniani kote, vijana ndio uhai wa Taifa. Hii ni kwa sababu wapo wengi; wana nguvu na uthubutu. Hivyo basi, katika Siku hii ya kilele cha Sherehe ya Wiki ya Vijana Kitaifa, napenda kuwahimiza vijana kote nchini kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu. Mtambue ya kuwa Taifa hili ni lenu. Na maendeleo yake yanawategemea ninyi.

Lakini ili kijana aweze kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa na kutoa mchango wenye tija kwa nchi, hana budi, kujiendeleza kielimu kila wakati na kujiepusha na vitendo vitakavyopunguza uwezo wake, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na ngono zembe. Na huo ndio wito wangu mwingine kwenu vijana wa Tanzania leo mnapoadhimisha kilele cha Wiki ya Vijana Kitaifa.

Waheshimiwa Mawaziri;

Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Nimesema mengi. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kuwashukuru tena Mawaziri husika kwa kunialika kwenye tukio hili. Aidha, nawashukuru tena wananchi wa Mjini Magharibi na Zanzibar kwa ujumla kwa mapokezi yenu mazuri na pia kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hili. Lakini shukrani za pekee ziende kwenye makundi yafuatayo:

Kwanza, kwa waandaji wa tukio hili. Shughuli imefana sana. Hongereni sana. Pili, natoa shukrani kwa viongozi wa dini wote ambao wametuombea dua na kuliombea Taifa letu. Tatu, natoa shukrani na pongezi nyingi sana kwa wakimbiza Mwenge wetu wa Uhuru mwaka huu wakiongozwa na Amour Hamad Amour. Mmefanya kazi kubwa sana. Hatuna cha kuwalipa.

Napenda pia kutoa shukrani zangu nyingi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha usalama unakuwepo hapa uwanjani na sehemu zote ambazo Mwenge ulipita. Nawashukuru pia Vijana wa Halaiki kwa kutuburudisha. Mmetia fora. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, navishukuru vyombo vya habari vyote vilivyoripoti tukio hili. Tunawashukuru sana.

Mwisho kabisa, kama mnavyofahamu, mimi pamoja na kuwa Rais, ni Mwenyekiti wa CCM. Natambua kuwa hapa kuna wana-CCM wengi. Na hivi sasa Chama chetu kipo kwenye zoezi muhimu la uchaguzi. Hivyo basi, napenda niwatakie wana-CCM wote uchaguzi mwema. Wito wangu kwenu, chagueni viongozi bora, wenye uwezo wa kuongoza, wasio makundi na wala kujihusisha na vitendo vya rushwa; ili Chama chetu kibaki kuwa imara. Mara zote tukumbuke wosia wa Baba wa Taifa wakati aking’atuka mwaka 1985, kuwa “Bila CCM imara, nchi itayumba”. Kidumu Chama cha Mapinduzi.

Napenda kuhitimisha kwa moja ya kauli za Baba wa Taifa, aliyoitoa kwenye Sherehe za Miaka 40 ya Uhuru wa Ghana zilizofayika tarehe 6 Machi, 1997 mjini Accra, nanukuu “Kizazi changu kiliongoza jitihada za kuleta uhuru wa kisiasa wa Bara letu. Kizazi cha sasa cha Waafrika hakina budi kuchukua kijiti pale tulipoishia, na kwa nguvu mpya, kusukuma mbele maendeleo ya Bara letu”, mwisho wa kunukuu. Hivyo basi, leo tunapokumbuka maisha ya Baba wa Taifa pamoja na falsafa ya Mwenge wa Uhuru, sisi Watanzania wa kizazi cha sasa, hatuna budi kukumbushana kuchukua kijiti kilichoachwa na waasisi wetu ili kulipeleka Taifa letu mbele zaidi, hasa kiuchumi.

Mungu Ibariki Familia ya Baba wa Taifa!

Mungu Ibariki Familia ya Mzee Karume pamoja na Waasisi wote!

Mungu Ubariki Mwenge wa Uhuru!

Mungu Wabariki Vijana wote wa Tanzania!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”