Tanzania kupunguza matumizi ya Zebaki kwa asilimia 30 ifikapo 2024

Tanzania imepitisha Mpango Kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2024.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma katika kikao kilichoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kushirikisha sekta ya madini.

Zebaki imetajwa kuwa moja kati ya kemikali 10 hatarishi zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na ina madhara makubwa hasa kwenye magonjwa ya mfumo wa fahamu.

Tanzania inakadiriwa kuwa na wachimbaji wadogo milioni 1.2 ambapo asilimia 20 hadi 30 ni wachimbaji wanawake huku sehemu kubwa ya wachimbaji hao hutumia zebaki na inakadiriwa mwaka tani 13 hadi 24 hutumika na huingizwa nchini kinyemela.

Zaidi ya asilimia 25 hadi 33 ya wachimbaji wadogo wadogo wameathirika na matumizi ya zebaki hivyo Serikali imedhamiria kupunguza  ama kuondosha matumizi yake kwa wachimbaji wadogo.

Wakizungumza mara baada ya kumaliza kikao hicho Mdau wa madini, Noela Magoche alitaka zifikiriwe mbinu mbadala kunusuru watoto wanaofanya kazi migodini.

Alisema watoto ndio waathirika wakubwa wa zebaki huku akisisitiza itekelezwe sheria inayokataza  ajira kwa watoto.

Kwa upande wake Mdau mwingine wa mazingira, Haji Rehani alisema zebaki imetambulika kimataifa kwa kuwa na madhara ya kiafya.