TAMKO LA KATIBU MKUU JUU YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI 2019

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

TAMKO LA MHANDISI JOSEPH K. MALONGO KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS   KWA VYOMBO VYA HABARI KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI TAREHE 5 JUNI, 2019

Ndugu Wananchi,

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni. Watanzania wanaungana na nchi nyingine duniani kote kuadhimisha siku hii ambayo iliamuliwa na mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu mazingira. Mkutano huo ulifanyika nchi Sweden katika mji wa Stockholm mnamo tarehe 5-16 Juni,1972. Madhumuni makubwa ya maadhimisho haya ni kuelimisha jamii kuchukua hatua kulinda na kuhifadhi mazingira ya maeneo yao. Kuhamasisha jamii  kufahamu wajibu wao wa kuhifadhi mazingira.

 Ndugu Wananchi,

Kaulimbiu ya kimataifa ya maadhimisho haya ni Uchafuzi wa Hewa” (Air Pollution). Kaulimbiu hii imechaguliwa kutokana na uchafuzi wa hewa ambao unatokana na maendeleo ya viwanda hapa duniani.  Aidha, uchafuzi wa hewa una madhara makubwa kwa afya ya binadamu kwani husababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo ya mapafu, kichwa na macho. Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Mataifa umeona ni vema kuwepo kwa kaulimbiu hii ili kuhimiza nchi zote duniani kupunguza shughuli zinazosababisha uchafuzi wa hewa. Kutokana na kaulimbiu hii China imechaguliwa na Umoja wa Mataifa kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya kwa kuwa imepunguza shughuli zinazochangia uchafuzi wa hewa kwa kuwa na magari yanayotumia nishati ya umeme. Hivyo kupeleka maadhimisho haya China kunatoa fursa kwa nchi nyingine duniani kujifunza kutoka China kupunguza shughuli zinazochangia uchafuzi wa hewa.

Kutokana na Serikali yetu kupiga marufuku mifuko ya plastiki na kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala, imeamua kaulimbiu ya kitaifa ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu iwe;- Tumia mifuko mbadala wa Plastiki; kwa Ustawi wa Afya, Mazingira na Maendeleo ya Uchumi”. “Kaulimbiu inahamasisha jamii kuacha kuzalisha kuingiza ndani ya nchi kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki. Aidha kaulimbiu inahamasisha wananchi kutumia mifuko mbadala. Aidha, kutokana na serikali kujikita katika kampeni hiyo, imeamuliwa kuwa hapatakuwepo na maadhimisho ya kitaifa na badala yake kila Mkoa utafanya maadhimisho haya katika maeneo yake kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu. Mikoa imeelekezwa kuendelea kukusanya mifuko ya plastiki na kuipeleka kwenye maeneo yaliyobainishwa ili kufanyiwa taratibu za kuirejeleza.

 Ndugu Wananchi,

Nia ya kutokomeza mifuko ya plastiki ni ya dunia nzima, kwa kutambua hilo Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira  liliazimia kuwa uchafuzi wa mazingira utokanao na taka za plastiki ukomeshwe na hadi sasa, zaidi ya nchi 100 duniani zikiwemo nchi 25 kutoka Bara la Afrika zimechukua hatua mbalimbali kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki. Baadhi ya nchi za jirani kama vile Rwanda na Kenya ambazo zimeshapiga marufuku mifuko hii zinadhihirisha ukweli huu. Ili kufanikisha zoezi la kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki serikali inaendelea kuhamasisha jamii kuzalisha kwa wingi mifuko mbadala kwa lengo la kukidhi haja ya uhitaji uliopo. Kwa kuwa suala la hifadhi ya mazingira ni jukumu letu sote, kila mmoja anahimizwa kuacha kutumia mifuko ya plastiki na kuanza kutumia mifuko mbadala.

Ndugu Wananchi,

Aidha, hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki itaibua fursa mpya za ajira na kipato kwa viwanda, vikundi vidogo vidogo na wajasiriamali katika uzalishaji wa vikapu vya asili na mifuko mbadala ya karatasi, nguo, katani na mingineyo.

Tunavipongeza vyombo vya habari nawadau mbalimbali wa Mazingira kama vile UNEP, WWF, na wengine kwa kushirikiana na Serikali kuhamasisha jamii kutokomeza mifuko ya plastiki.

MHANDISI JOSEPH MALONGO

KATIBU MKUU

OFISI YA MAKAMU WA RAIS