TAMASHA LA ‘TULONGE MAZINGIRA NA MIMI’ LAFANA

Tamasha kubwa lililopewa jina la “Tulonge Mazingira na Mimi” limefanyika mwishoni mwa wiki katika Viwanja vya Mbagala Zakhem Jijini Dar es Salaam. Tamasha hilo la aina yake lilipambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na lililenga kukuza uelewa wa wananchi juu ya hifadhi ya mazingira msisitizo ukiwa ni kutumia nishati mbadala wa Mkaa kama kauli mbiu ya Siku ya Mazingira kwa mwaka huu inavyosema.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika viwanja hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema wananchi wana wajibu mkubwa katika kuhifadhi mazingira na kuwataka kuwa mstari wa mbele kuuliza viongozi wao ni nini wanafanya kuhusu mazingira. “Tuulizeni kuhusu Mazingira na nini tunafanya kuhusu hifadhi ya mazingira” Makamba alisisitiza.

Aidha Mhe. Makamba ameitaka jamii kutoa taarifa juu ya mtu yeyote anaechafua mazingira katika maeneo yao kwani Sheria ya Mazingira inatoa nafasi hiyo ya kumshtaki mtu yoyote. “Sheria ya mazingira  Kifungu cha 5 kimewapa wananchi nguvu ya kushtaki kwa niaba yake kama yanaharibiwa, maana kila mtu ni mdau katika suala la mazingira,  hivyo msilalamike badala yake chukueni hatua stahiki pale mazingira yanapoharibiwa katika maeneo yenu” Makamba alisisitiza.

Wakati huo huo, Waziri Makamba ameagiza kila mtaa, kijiji na  kitongoji katika nchi yetu kuwa na Kamati ya Mazingira ambayo kisheria ina nguvu kubwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha upelelezi kwenye jambo lolote, kufunga na kufungia kitu chochote kwenye mtaa kinachoharibu mazingira.

Kampeni hiyo ya kuhifadhi mazingira itaendelea nchi nzima na imeambatana na utoaji wa tuzo za hifadhi ya Mazingira ngazi ya Mkoa, tuzo zilizotolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Felix Lyaviva. Tamasha hilo pia limehudhuriwa na viongozi wa mbalimbali wa Serikali, Wabunge na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.