TAARIFA MAALUM YA MIAKA 55 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

 

 

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 

 

 

 

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

TAARIFA MAALUM YA MIAKA 55 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais

April, 2019

 

DODOMA.

 

TAARIFA MAALUM YA MIAKA 55 YA MUUNGANO WA

TANGANYIKA NA ZANZIBAR

 

 

1.0       UTANGULIZI

Leo tarehe 26 Aprili, 2019 Muungano wetu umetimiza miaka 55 yenye maendeleo katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yanayonufaisha wananchi kwa kuwapa fursa za kuishi kwa amani na kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni jambo linalojidhihirisha kuwa Muungano wetu umeendelea kudumu na kimsingi umekuwa nyenzo na utambulisho muhimu wa umoja wetu.

 

2.0       MAFANIKIO

Muungano huu umedumu kutokana na dhamira za dhati za umoja waliokuwa nao Waasisi watu, sera makini za Serikali zote mbili za TANU na ASP na sasa CCM, jitihada

zinazoendelezwa na viongozi waliofuatia baada ya Waasisi pamoja na kuungwa mkono na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zaidi ya yote, utamaduni wa kukaa na kuzungumzia changamoto kila zinapojitokeza na kuzitatua kwa pamoja kwa kuzingatia misingi ya umoja na mshikamano vimeimarisha na kuufanikisha Muungano wetu.

 

Katika kipindi cha Miaka 55 ya Muungano, tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia, Watanzania wamejenga umoja na misingi endelevu ya udugu baina yao, ikiwa ni uthibitisho kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaendelea kuimarika. Kwa kutumia misingi iliyowekwa, wananchi na viongozi wanahakikisha kwamba uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar vinaenziwa. Vile vile, pande mbili za Muungano zimejenga mifumo ya kuendesha Serikali zake kwa uwazi chini ya misingi ya demokrasia na utawala bora. Misingi hiyo imeimarika kutokana na uelewa mzuri wa dhana ya uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi zote.

 

Uchumi umekua kwa kiwango cha kuridhisha, kipato cha kila mwananchi kimeongezeka na mfumuko wa bei umedhibitiwa. Aidha, tumeshuhudia kuimarika kwa miundombinu ya barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini na kuimarika kwa huduma za jamii.  Pia, tumeendelea kutumia maliasili zetu vizuri zaidi kwa manufaa ya wananchi wa pande mbili za Muungano kuliko ilivyokuwa kabla ya Muungano. Mafanikio hayo yametokana na usikivu, utulivu, uzalendo, moyo wa kujituma na kujitolea na ushirikiano wa dhati wa viongozi na wananchi wote wa pande mbilkiza Muungano.

 

Tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuasisiwa mwaka 1964, Serikali zetu  mbili zimeendelea na jitihada za makusudi za kuhakikisha kuwa masuala yanayoleta vikwazo katika Muungano yanashughulikiwa. Aidha, Serikali zimeweka utaratibu wa wataalam na viongozi wa kisiasa kukutana na kujadili masuala yanayoonekana kuwa ni vikwazo na kutoa ushauri. Pia,  utaratibu mwingine ni ule wa kuunda Tume na Kamati ili kuisaidia Serikali katika kushughulikia changamoto hizo.

 

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 55 ni pamoja na:-

 

 1. Sheria nyingi kutungwa au kurekebishwa kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa mambo ya Muungano, kwa mfano:- Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria Na.13 ya 1995; Sheria ya Uhamiaji Na. 6 ya mwaka; Sheria ya Mamlaka ya Kodi Na. 11 ya 1995; Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania Na. 1 ya 1995; Sheria ya Tume ya Pamoja na Fedha Na. 14 ya 1996; Sheria ya Biashara ya Bima ya Tanzania Na.18 ya 1996; Sheria ya Usalama wa Taifa Na. 15 ya 1996; Sheria ya Uraia Na. 6 ya 1995; na Sheria ya Usalama wa Taifa Na. 15 ya 1995. Aidha, Sheria namba 34 ya mwaka 1994 iliyoanzisha Ofisi ya Makamu wa Rais na kumpatia jukumu lingine la kuratibu ushirikiano katika masuala yasiyo ya Muungano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lengo ikiwa ni kuimarisha masuala yasiyo ya Muungano ya pande mbili za Muungano;
 2. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufungua akaunti yake Benki Kuu na kuendelea kupata huduma za kibenki ikiwemo mikopo na ushauri wa kitaalam juu ya kukuza uchumi kwa wananchi wa Zanzibar. Aidha, Tawi la Benki Kuu limejengwa Zanzibar ili kusogeza huduma karibu na wananchi;

 

 • Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa ya kudumisha amani na kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo. Jeshi hili limeundwa na askari toka pande mbili za Muungano ambao wanafanya kazi kwa ushirikiano;

 

 1. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imefungua Ofisi ndogo Zanzibar;

 

 1. Uratibu wa masuala ya ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili umeendelea kuimarisha Muungano kwani umewekwa Mwongozo wa vikao vya kisekta ambavyo vinasimamiwa na kuratibiwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar;

 

 1. Kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu na faida za Muungano kwa umma wa watanzania kuhusu Muungano wetu. Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na jitihada za kuelimisha umma kuhusu Muungano kupitia Redio, Televisheni, Magazeti, Semina, Warsha, Makongamano, Maonesho ya Kitaifa, Ziara na machapisho;

 

 • Miradi ya maendeleo imebuniwa na kutekelezwa na Serikali zetu mbili ili kunufaisha wananchi wake. Utekelezaji wake umekuwa na matokeo endelevu katika nyanja zifuatazo:- Elimu; Afya; Masoko; Maji; Mazingira pamoja na Usafiri na Usafirishaji. Miongoni mwa miradi na programu zilizowahi kutekelezwa pande mbili za Muungano na kukamilika ni pamoja na:-
 • Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tanzania Social Action Fund – TASAF ) TASAF I, TASAF II na TASAF III;
 • Programu ya Usimamizi wa Bahari na Pwani (Marine and Coastal Environmental Management Programme – MACEMP);
 • Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Sekta ya Mifugo (Agricultural Sector Development Program – ASDP);
 • Agricultural Sector Development – Livestock – ASDP – L, Agricultural Sector Support Program – ASSP;
 • Programu ya Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Account Tanzania – MCA – T); na
 • Mradi Shirikishi wa Programu za Maendeleo ya Kilimo (Participatory Agricultural Development Program – PADEP).
 • Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (Expanded Rice Production Project – ERPP);
 • Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Maeneo ya Pwani- LDCF;
 • Mradi wa Udhibiti wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi – SWIOFISH;
 • Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA);
 • Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (Market Infrastracture, Value Addition and Rural Finance – MIVARF); na
 • Miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.

 

Miradi na programu hizo zinazingatia viashiria vya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals – MDG) 2020 – 2025 na Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi  ya CCM ya mwaka 2015 -2020 kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji wa jamii.

 • Utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO) na kufuta malimbikizi ya deni la kodi ya VAT lililofikia shilingi bilioni 22.9 kwa TANESCO kwenye umeme uliouzwa ZECO.
 1. Ujenzi wa Ofisi pande zote mbili za Muungano lengo ikiwa ni kusogeza huduma kwa watanzania wote. Ofisi hizo ni pamoja na:- Ofisi ya Makamu wa Rais, Mtaa wa Luthuli, Dar es Salaam; Ujenzi wa Ofisi na Makazi ya Makamu wa Rais Tunguu, Zanzibar; Ujenzi wa Tawi la Benki Kuu – Gulioni, Zanzibar; Ofisi ya Uhamiaji, Zanzibar; Ofisi ya Bunge Tunguu, Zanzibar; Makao Makuu ya Mamlaka ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu – Fumba, Zanzibar; na Taasisi ya Sayansi za Bahari –Buyu, Zanzibar. Ofisi zingine zilizoanzishwa ni:- Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Kikwajuni, Zanzibar; TANTRADE na NIDA zimefungua ofisi zake Zanzibar; Sekretarieti ya Ajira, Shangani, Zanzibar;  TAEC na COSTECH  pia zimefungua Ofisi Maruhubu, Zanzibar;
 2. Ongezeko kubwa la huduma za usafiri wa anga na wa majini kati ya Tanzania Bara  na Tanzania Zanzibar.  Wananchi wa pande zote za Muungano  wamekuwa wakitembeleana kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ya Muungano bila kubaguliwa  au kusumbuliwa, jambo ambalo limeimarisha  umoja na mshikamano wetu hivyo kudumisha Muungano na uhusiano wa karibu baina ya pande hizi mbili.

 

3.0       CHANGAMOTO

Muungano umepitia vipindi vyenye matukio mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyotokea ndani na nje ya nchi na ambayo kwa njia moja au nyingine, yaliathiri uendeshaji wa shughuli za Muungano. Miongoni mwa hayo ni:-

 1. Kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1967;
 2. Kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977;
 3. Vita dhidi ya Iddi Amini wa Uganda mwaka 1979;
 4. Kuyumba kwa uchumi wa Dunia miaka ya 80;
 5. Kulegezwa kwa masharti ya biashara na kuanzishwa sera ya uchumi huria; na
 6. Kuanzishwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa mwaka 1992.

 

Changamoto nyingine ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii ya Watanzania kuhusu masuala ya Muungano na utekelezaji wake. Mifumo tofauti wa Sheria ya pande mbili za Muungano hukwamisha utekelezaji wa baadhi ya maamuzi yanayofikiwa katika kutatua vikwazo vya Muungano.

 

4.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa tangu mwaka 1964 kutatua changamoto hizo kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza Muungano wetu. Hatua hizo ni pamoja na:-

 1. Kuundwa kwa Tume na Kamati mbalimbali ambazo zilitoa maoni na mapendekezo ya kuboresha na kuuendeleza Muungano wetu.  Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano ambayo inatumia utaratibu wa vikao katika kutatua changamoto zinazoukabili Muungano wetu.

Tangu mwaka 2006, vimefanyika vikao kumi (11) vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ. Vikao hivi vilitanguliwa na vikao vya Mawaziri, Makatibu Wakuu na wataalamu wa kisekta kutoka Serikali zote mbili.

 

Katika kipindi hiki, hoja kumi na tano (15) ziliwasilishwa na kujadiliwa, kati ya hoja hizo, kumi na moja (11) zimetatuliwa na hoja nne (4) ziko katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi. Hoja zilizopatiwa ufumbuzi ni:-

 1. Utekelezaji wa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora;
 2. Utekelezaji wa Merchant Shipping Act katika Jamhuri ya Muungano na Uwezo wa Zanzibar Kujiunga na International Maritime Organisation (IMO);
 3. Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu;
 4. Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
 5. Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kukopa Ndani na Nje ya N chi;
 6. Wafanyabiashara wa Zanzibar kulalamika kutozwa Kodi Mara Mbili;
 7. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT);
 8. Ongezeko la Gharama za Umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO;
 9. Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Kimataifa;
 10. Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano; na
 11. Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.

Hoja zilizo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi ni:-

 1. Mgawanyo wa mapato ya kodi na misaada;
 2. Usajili wa vyombo vya moto;
 3. Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu; na
 4. Taarifa ya mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha.

 

Aidha, Kamati ya Pamoja ya  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Kushughulikia Masuala ya Muungano imeendelea na kutafuta njia mbalimbali za kuhakikisha Muungano wetu unaendelea kuimarika kwa kuanzisha Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja wenye lengo la kuimarisha na kuongeza ufanisi wa kufuatilia maagizo na maelekezo yanayotolewa na Kamati hiyo kwa ajili ya mustakabali wa Watanzania wote.

 

 

 

6.0       HITIMISHO

Ofisi itaendelea na majukumu yake ya Kikatiba  na Kisheria ya kuratibu shughuli za Muungano na kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, katika jitihada za kuondoa vikwazo katika utekelezaji wa masuala ya Muungano, Ofisi itaendelea kuratibu vikao vya ufumbuzi wa hoja za Muungano, kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, majarida, na maonesho mbalimbali ya Kitaifa, kuhimiza ziara za kisekta ili kuimarisha ushirikiano wa Serikali zetu mbili.

 

Mafaniko yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 55 ya Muungano, yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya viongozi na wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Mafanikio hayo siyo ya kubezwa hata kidogo na yanapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa nguvu zote. Hivyo, ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha kuwa anaulinda, anauenzi na anaudumisha Muungano wetu.

 

 

 

January Y. Makamba (Mb.)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira