Taarifa kwa Umma

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ndugu January Makamba (Mb), leo anaanza ziara ya mikoa 19 nchini, ambayo itafanyika kwa awamu tatu. Ziara hiyo inamadhumuni yafuatayo:-

  1. Kukagua, kutathmini na kuzungumza na viongozi, wataalam, watendaji na wananchi wa mikoa husika kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

Kama inavyofahamika, Sheria ya Mazingira, hasa vifungu vya 47, 51, 54, 56, na 58 (3), inatoa mamlaka kwa Waziri mwenye dhamana ya mazingira kutangaza, kutamka au kuamuru, kupita kwenye Gazeti la Serikali, baadhi ya maeneo nchini kuwa ni Maeneo Lindwa Kimazingira (Environmental Protected Area) au Maeneo Nyeti Kimazingira (Environmental Sensitive Area). Nyenzo hizi zimewekwa ili kuyalinda maeneo muhimu kwa mifumo ya kiikolojia (ikiwemo vyanzo vya maji, mito, maziwa, mabwawa, milima na vilima, chemichemi, ardhi oevu, mazalia ya samaki, misitu, nk.) ambayo hayana ulinzi wa Sheria nyingine. Sheria imeweka vigezo kwa maeneo hayo. Ofisi ya Makamu wa Rais, kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), iliomba na kupokea kutoka katika Halmashauri mbalimbali nchini mapendekezo ya maeneo hayo. Jumla ya maeneo 77 yalipendekezwa, ikiwemo vyanzo muhimu vya maji, mazalia ya samaki na wanyama adimu, maeneo ya ardhi oevu, mabwawa, mito na chemichemi nyeti. Mikoa iliorodhesha maeneo hayo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Sheria. Katika awamu ya kwanza, maeneo takriban 20 yanatarajiwa kuhifadhiwa kwa kutumia Sheria ya Mazingira.

Katika ziara yake,  Ndugu Makamba anatarajia kuyaona maeneo hayo, kutathmini hoja na haja ya kuyahifadhi na kuzungumza na viongozi wa mikoa, halmashauri na wananchi katika maeneo hayo ilikubaini utayari na uwezo wao katika kusimamia uhifadhi mara maeneo hayo yatakapotangazwa. Vilevile, katika ziara hiyo, Ndugu Makamba atapokea mapendekezo ya maeneo mapya hasa pale ambapo mapendekezo yaliyotolewa awali hayakutokana na ushirikishwaji mpana. Orodha ya maeneo yanayopendekezwa itatolewa kadri ziara inavyoendelea katika kila mkoa.

Awamu ya kwanza ya ziara hii, ambayo inaanza leo tarehe 20 Agosti hadi tarehe 6 Septemba 2018, inajumuisha mikoa ya Singida, Tabora, Simiyu, Geita, Mwanza, Mara, Arusha, na Manyara.

  1. Kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi Mazingira ya 2004 katika ngazi za Serikali za Mitaa.

Kama inavyofahamika, Sheria ya Mazingira pia imeweka taratibu na mifumo, ikiwemo ya kitaasisi, ya kusimamia hifadhi ya mazingira nchini na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira. Sheria pia imeweka wajibu kwa mamlaka mbalimbali, ikiwemo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Vifungu kuanzia 34 hadi 42 vya Sheria ya Mazingira vinahusu wajibu wa Sektretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika ziara yake, Ndugu Makamba pia atajionea na kuzungumza na viongozi wa mikoa na halmashauri mbalimbali katika mikoa hiyo ili kusaidiana nao na kuhakikisha kwamba matakwa ya Sheria kwa upande wa wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwemo uundwaji wa Kamati za Mazingira katika ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa,yanatimizwa.

 

Katika ziara  hii, Waziri Makamba ataongozana pia na watendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuangalia namna ya kuwezesha makubaliano kati ya NEMC na halmashauri mbalimbali katika mikoa yote kuhusu masuala kadhaa ya ukaguzi na ufuatiliaji wa hifadhi ya mazingira.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Ofisi ya Makamu wa Rais

20 Agosti 2018