Simbachawene aonya wanaotumia mifuko milaini ya plastiki

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene ameonya kuwa Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayekutwa akibebea bidhaa mifuko milaini myeupe ya plastiki.

Mhe. Simbachawene alitoa onyo hilo Agosti 15 alipofanya ziara katika Soko Kuu la Kariakoo Jijini Dar es Salaam ambapo alishangazwa na kuendelea kuuzwa kwa mifuko hiyo pamoja na kupigwa marufuku na Serikali.

Waziri alibainisha kuwa kuendelea kutumika kwa mifuko hiyo milaini kinawafanya wazalishaji wa mifuko mbadala kuvunjika moyo kuendelea kuizalisha.

Aliongeza kuwa ipo mifuko mbadala ikiwemo ya karatasi au vikapu inaweza kutumika na kuwataka kuacha mara moja kutumia mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na Serikali tangu Juni mosi.

Aidha Waziri Simbachawene aliwapa siku 14 wafanyabiashara katika soko hilo wanaodaiwa kuwa chimbuko la kuwepo kwa mifuko hiyo kuiondoa sokoni mara moja.

Kwa mujibu wa Sheria mtu yeyote atakayeingiza nchini, kusafirishaji nje ya nchi, kuzalishaji, kuuza, kusambaza, kuhifadhi na kumia mifuko ya plastiki atachukuliwa hatua kali za kisheria zikiwemo kifungo, faini ama vyote kwa pamoja.